Featured Kitaifa

TUME YA MADINI YAENDELEA KUTOA ELIMU KWA WADAU WA MADINI

Written by mzalendo

Tume ya Madini leo Julai 03, 2024 imeendelea kutoa elimu kwa wadau wa madini katika Maonesho ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Elimu imetolewa katika maeneo ya usimamizi/udhibiti wa Sekta ya Madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na tozo mbalimbali zinazotokana na shughuli za madini, utoaji na usimamizi wa leseni za utafutaji wa madini, uchimbaji na biashara ya madini pamoja na namna ya kujisajili katika mfumo wa Online Mining Cadastre Transaction Portal (OMCTP),ukaguzi na usalama wa migodi, afya, mazingira na njia bora ya uzalishaji wa madini kwa migodi midogo, ya kati na mikubwa.

Maeneo mengine ni pamoja na usimamizi wa biashara ya madini inayofanyika katika masoko ya madini yaliyoanzishwa nchini, ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini na wajibu wa wawekezaji kwa jamii katika uboreshaji wa huduma (Corporate Social Responsibity; CSR)

Aidha, elimu imelenga katika maeneo ya upatikanaji wa vibali mbalimbali vya kusafirisha madini ndani na nje ya nchi na huduma zinazotolewa na Maabara ya Tume ya Madini hususan upimaji wa madini ya metali.

Wakizungumza wadau mbalimbali waliotembelea banda la Tume ya Madini wamepongeza kazi kubwa inayofanywa na Tume kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini kupitia utoaji na usimamizi wa leseni za madini, usimamizi wa masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini nchini, usimamizi wa usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini.

About the author

mzalendo