Featured Kitaifa

MAAFISA USTAWI WATAKIWA KUSIMAMIA MASHAURI YA USTAWI NA AFYA KWA WAKATI

Written by mzalendo

Na WMJJWM, Mbeya

Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za Ustawi wa jamii kwa kutumia mikakati inayolenga kuleta mabadiliko katika Jamii ikiwemo kufanya ufuatiliaji na utafiti wa utoaji wa huduma hizo hususani kwa watoto na vijana.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis katika kikao kazi na watoa huduma za Ustawi wakati wa ziara yake ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa utafiti wa ustawi na afya ya watoto na Vijana Julai 03, 2024, mkoani Mbeya.

Mwanaidi amewasihi watoa huduma hususani Maafisa ustawi kuwa sehemu kubwa ya suluhisho na matumaini kwa wananchi wanaokuwa wanatafuta haki kupitia mifumo ya Serikali.

“Maafisa wote wanapaswa kukamilisha mnyororo wa kusimamia mashauri ya afya na ustawi yaliyopokelewa ili yafanyiwe kazi kwa utaratibu unaofaa na kwa wakati na mpango wa huduma kwa kila shauri ukamilike lakini pia taarifa za mashauri hayo ziwepo na ufuatiliaji wa mashauri haya” Alisema Mwanaidi.

Aidha, Mwanaidi amepongeza mkoa wa Mbeya kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utoaji wa huduma za Maendeleo na Ustawi wa Jamii ikiwemo usimamiaji wa ulinzi na usalama wa mtoto, uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na huduma kwa wazee na wenye ulamavu.

Huduma nyingine ni usajili na usimamizi wa vituo vya kulelea watoto na makao ya watoto pamoja na usimamiaji wa miradi mingine iliyo chini ya Idara ya Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Jamii

Kwa upande wake Kamishna msaidizi wa Ustawi wa Jamii Baraka Makona amewataka maafisa ustawi kutumia nafasi zao kutatua changamoto za kiustawi kwa kutumia rasilimali zilizopo akibainisha kuwa Serikali imejitahidi kwa kiwango kikubwa kutoa rasilimali za kutosha pamoja na mafunzo ili kukabiliana na mashauri hivyo ni muhimu kuacha kutumia kigezo cha upungufu wa rasilimali na kufanya kazi kama inavyotakiwa.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Ustawi na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Subisya Kabuje amesema Serikali imeendelea kukusanya na kutafuta rasilimali zitakazowawezesha maafisa Ustawi kusimamia shughuli zao za kutoa huduma ikiwemo kusimamia mashauri.

     

About the author

mzalendo