Featured Kitaifa

RAIS SAMIA ATATUA KILIO CHA WANANCHI WA MITIMIREFU

Written by mzalendoeditor

Na. Majid Abdulkarim, Siha

Serikali chini ya Uongozi imara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan umeipatia Kata ya Mitimirefu kiasi cha Shilingi Milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ili kutatua adha ya wanafunzi wa kata hiyo kutembea zaidi ya kilomita 14 kila siku kwenda shule.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Siha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Dkt Godwin Mollel wakati wa ziara yake Jimboni akizungumza katika mkutano na wananchi wa Kata ya Mitimirefu leo Julai 03, 2024 baada ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa jimboni kwake ikiwemo ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi, ujenzi wa chuo cha ufundi stadi VETA na ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya msingi Namwai.

Dkt. Mollel amesema changamoto ya kutembea umbali mrefu, kukwepa wanyama wakali, kuacha shule na mimba za utotoni zilizokuwa sikisababishwa na ukosefu wa shule ya sekondari katika Kata ya Mitimirefu zitamalizika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya MItimirefu.

“Serikali chini ya Uongozi imara na sikivu Rais Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wananchi wa Mitimirefu na wapigakula wake wa jimbo la Siha hivyo amekubali kuleta fedha za kujenga shule mpya ili watoto wapate ambao ni taifa la kesho waweze kutimiza ndoto zao kwa elimu bora katika mazingira bora”, ameeleza Dkt. Mollel.

Hata hivyo Dkt. Mollel ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali yao kwa kuongeza nguvu kazi kama kuchimba msingi na kujaza vifusi ili utekelezaji wa mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kama iliyokusudiwa na serikali yao sikivu.

“Mmenituma nikafanye kazi ili kuletea maendeleo ya Wilaya ya Siha, na tunapohakikisha watoto wanapata elimu bora katika maeneo yao ni maendeleo, tunapowajengea Zahanati ni maendeleo, tunapojenga barabara na kuwaletea maji karibu ni maendeleo hivyo hatuna budi kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ili azidi kutufanyia zaidi ya hapa” amesisitiza Dkt. Mollel.

Aidha Dkt. Mollel amefanya ziara jimboni kwake ya kukagua miradi ya maendeleo ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi, ujenzi wa chuo cha ufundi stadi VETA na ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa shule ya msingi Namwai, ujenzi wa Zahanati ya Mitimirefu, kukagua hali ya utoaji wa huduma za afya na kuongea na watumishi wa Wilaya ya Siha.

Hata hivyo amewapongeza watumishi wote wa wilaya ya Siha kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuwahudumia wananchi pamoja na kusimamia fedha ya miradi inayoletwa na serikali ili wanachi waweze kupata huduma bora.

About the author

mzalendoeditor