Featured Kitaifa

SERIKALI NA JWT WAAFIKIANA KUSIMAMIA MAAZIMIO 15 NA KUTOA MAAGIZO KWA TRA

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Serikali pamoja na uongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara nchini (JWT) wameafikiana kusimamia maazimio 15 ambayo ndani yake serikali imetoa maagizo kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kusitisha Mara moja mazoezi yote ya kamata kamata pamoja na kusitisha mazoezi mengine yote ya ufuatiliaji wa risisti za EFD katika maeneo yote nchini hadi mwezi Agosti, 2024.

Hayo yameelezwa leo Juni 27,2024 na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali Thobias Makoba wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao baina ya Serikali na uongozi wa jumuiya ya wafanyabiashara nchini huku akiongeza kuwa pamoja kusitishwa huko wafanyabishara wanahimizwa kuelendelea kutoa risiti za mauzo.

Amesema mazungumzo hayo yalitokana na madai na hoja takribani 41 ambazo wafanyabiashara waliziwasilisha serikalini ikiwa ni sehemu ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini.

“Kutokana na hoja hizo, na baada ya vikao na mawaziri wa sekta husika, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia falsafa ya R 4 za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ile ya Reconciliation kwa maana ya maridhiano amehitimisha mazungumzo hayo hapa Dodoma”, amesema.

Pia ameongeza kuwa TRA inaelekezwa kubainisha na kusimamia vyema orodha ya bidhaa nane ambazo zitawekewa bei elekezi kama ilivyo katika bidhaa za magari yaliyotumika ambapo bidhaa hizo ni Vitenge, Mashati, nguo nyingine, vipodozi, vito vya thamani, nguo za ndani, leso na vesti;

“Serikali kwa ujumla itaendelea na zoezi la kuwapanga na kuwawekea mazingira rafiki wafanyabiashara wadogo ambao hawako kwenye maeneo rasmi ili kurahisha usimamizi, ufuatiliaji na urasimishaji wao wa biashara”,ameongeza.

About the author

mzalendo