Featured Kitaifa

MABORESHO YALIYOFANYWA NA TANROADS KWENYE MIZANI YADHIBITI MIANYA YA RUSHWA-MHANDISI KYAMBA

Written by mzalendoeditor

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TANROADS imekamilisha ujenzi wa Mzani mpya wa kisasa wa Mikumi uliopo barabara kuu ya Morogoro – Iringa, pamoja na maboresho katika mizani ya mikese uelekeo wa barabara ya Dar-es Salaam – Morogoro kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9, hatua ambayo imesaidia kumaliza msongamano wa magari katika barabara hizo.

Baada ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji na Usafirishaji katika barabara ya TANZAM Highway Serikali iliona Mzani uliopo kuwa hautoshelezi mahitaji ya kupima magari kwa wingi, hivyo iliamua kufanya maboresho ya mzani uliopo pamoja na kujenga Mzani mwingine mpya na wa kisasa ili kuendana na mahitaji ya sasa.

Maboresho hayo yameenda sambamba na kuweka vifaa maalum (Sensor) ambavyo vitafanya kazi ya kuchuja na kutoa taarifa ya uzito wa gari husika, kama limezidisha mzigo ama la na kama halikuzidisha basi linaendelea na safari moja kwa moja bila kupita katika Mzani na lile lililozidisha mzigo litalazimika kupita kwenye mzani.

Ili kukabiliana na vitendo vya rushwa serikali kupitia TANROADS iliamua kujikita kwenye utengenezaji wa teknolojia kwa kufunga mifumo ya CCTV kamera na mifumo ya usimamizi wa taarifa kwenye maeneo yenye mizani za kupima uzito wa magari barabarani jambo ambalo kwa sasa kadhia ya rushwa imepungua kwa kiasi kikubwa kama sio kumalizika kabisa.

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania TANROADS wa mkoa wa Morogoro Mhandisi Alinanuswe L. Kyamba ameyasema hayo leo tarehe 23 Juni 2024 mara baada ya kutembelea na kukagua shughuli za ufanyaji kazi zinazofanywa katika Mzani wa Mikumi katika barabara ya Morogoro-Iringa, Mzani wa Dakawa barabara ya Morogoro-Dodoma na Mzani wa Mikese barabara ya Morogoro-Dar es salaam.

Mhandisi Kyamba amesema kuwa kwa sasa kwenye uendeshaji wa Mizani inatekelezwa sheria ya Jumuia ya Afrika Mashariki iliyoanza kutumika mwaka 2019 mwezi Machi ya namna ya udhibiti wa mizigo na kuzilinda barabara ziwe salama wakati wote, ambapo kwa sasa elimu inayotolewa imewezesha wasafirishaji wengi kufuata sheria na hivyo kusababisha idadi ya magari yanayozidisha uzito kupungua.

Amesema kuwa mifumo hiyo imewezesha shughuli zote za mizani kufanyika kwa uwazi, ambapo Meneja wa TANROADS wa Mkoa husika ataweza kuona kile kinachofanyika kwenye kituo chake cha mzani.

Ameomgeza kuwa kupitia mifumo hiyo TANROADS Makao Makuu na Wizara ya Ujenzi ina uwezo pia wa kuona kile kinachofanyika kwenye mzani na pale itakapobainika kuna uvunjivu wa sheria au viashiria vya rushwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi watu wanaohusika na vitendo vya rushwa.

Mhandisi Kyamba amewapongeza wafanyakazi wa mizani kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya usiku na mchana lakini amewasihi kuendelea kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kulinda miundombiniu ya barabara na kufanya kazi kwa tija.

About the author

mzalendoeditor