Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Elimu) Dkt. Charles Msonde amewataka wasimamizi wa Mradi wa Kupunguza Umaskini TASAF awamu ya nne kusimamia Mradi huo kwa weledi na kuhakikisha utekelezaji wa mradi huo unakuwa kama ilivyokusudiwa.
Dkt. Msonde ametoa maelekezo hayo mkoani Mwanza wakati akifungua kikao kazi cha mradi wa kupunguza umasikini awamu ya nne kilichofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Mwanza.
“Rais wa Awamu ya sita Mhe. Samia Suluhu Hassan alipotoa maelekezo kuhusu matumizi ya fedha kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa katika hafla iliyofanyika tarehe 10 Oktoba 2021 Jijini Dodoma, alieleza kwa undani umuhimu wa kuweka mkazo zaidi katika kutekeleza miradi ya huduma za elimu, afya na maji na kuondoa umaskini wa kipato ili kuziwezesha kaya nyingi maskini kutoka kwenye maisha ya utegemezi” amesema
Dkt. Msonde amesisitiza kuwa utekelezaji wa Mradi wa Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne, katika halmashauri unapaswa uendeleze na kuimarisha dhana ya uwazi, ukweli, ushirikishwaji na uwajibikaji.
Ameongeza kuwa Kazi za utekelezaji wa miradi unaoendelea katika Halmashauri zote za Mikoa mitatu ya Mwanza, Geita na Simiyu utekelezwe kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizopo za Mradi na Serikali, pamoja na wadau wanaofadhili Mradi unapoelekea kumaliza muda wa utekelezaji Machi 2025.
“Ningependa kuchukua fursa hii pia kuwakumbusha washiriki wa Kikao kazi hiki kuhusu utekelezaji wa miradi hii ya kupunguza umasikini kwa kufuata utaratibu wake uliowekwa katika maeneo yote ikiwemo ushirikishaji wa jamii katika hatua zote.
Akizungumza kwa naiba ya kamati ya uongozi ya TASAF,mwenyekiti wa kamati hiyo Peter Ilomo amesema watafanyia kazi maelekezo hayo na kuahidi kufanya ufuatiliaji wa mradi huo kwa karibu.
Mradi huu unalenga kupunguza umaskini kwa watu takriban milioni 3.1 katika Halmashauri 33 za Mikoa ya Njombe, Arusha, Simiyu, Geita na Mwanza.