Uncategorized

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA TAASISI YA AFYA YA KANDA YA AFRIKA MASHARIKI , KATI NA KUSINI

Written by mzalendo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ni muhimu kuimarisha mifumo ya Afya katika ngazi zote hususani huduma za afya ya msingi ili kudhibiti hatari za kiafya katika jamii.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Taasisi ya Afya Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Gran Melia Jijini Arusha. Amesema katika ukanda unaohudumiwa na Taasisi hiyo, ipo haja zaidi ya kuimarisha utayari wa kukabiliana na dharura za kiafya, namna ya kukabiliana, uhimilivu na urejeshaji hali ya kawaida baada ya changamoto ili kupunguza athari za dharura ya afya kwa umma na majanga ya kiafya katika ukanda huo.

Makamu wa Rais amesisitiza hitaji la kuongeza tafiti za kina za afya ambazo zitaweza kupelekea utambuzi bora wa magonjwa, chaguzi bora zaidi za matibabu na uimarishaji wa jumla wa mifumo ya afya. Amehimiza Katika miaka 50 ijayo, Nchi Wanachama wa ECSA–HC kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika tafiti za matibabu ya kibaiolojia, kliniki, utafiti wa kijamii, kitamaduni, mazingira na tafiti za kiafya za ongezeko la idadi ya watu.

Aidha Makamu wa Rais ametoa wito kwa nchi wanachama wa Taasisi ya Afya Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) kutafsiri kwa vitendo ahadi za kuongeza bajeti za sekta ya afya hususani bidhaa muhimu za matibabu, teknolojia pamoja na mifumo ya taarifa za afya ili kufikia viwango vya juu zaidi vya ustawi wa kimwili, kiakili na kijamii wa wananchi.

Amesema pamoja na kufikisha miaka 50 ya Taasisi hiyo, ni muhimu kushughulikia kwa pamoja changamoto na mapungufu yaliojitokeza ikiwemo ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari na shinikizo la damu. Ameongeza kwamba katika kukabiliana na changamoto hizo ni muhimu kuhusisha sekta zote muhimu na sio sekta ya afya pekee ikiwemo kusisitiza lishe bora pamoja na ufanyaji wa mazoezi.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuwa imara katika kutekeleza majukumu yake kwa Taasisi ya Afya Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika na kuwasihi washirika wote wa maendeleo kuendelea kuunga mkono ajenda za kipaumbele za Taasisi hiyo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amezishukuru serikali za nchi wanachama kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya licha ya uwepo wa vipaumbele vingi katika mataifa hayo. Amesema kwa miaka mingi mapendekezo mbalimbali yamepitishwa kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya na ustawi wa watu.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mawaziri wa Afya, wadau wa sekta ya Afya na Wataalam mbalimbali kutoka Mataifa ya Afrika.

Taasisi ya Afya Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika (ECSA-HC) ilianzishwa mwaka 1974 kwa lengo la kukabiliana na changamoto za Afya kwa pamoja.

About the author

mzalendo