Na Mwandishi Wetu, Tabora
Wakala ya Barbara za Vijijini na Mijini (TARURA ) mkoani TABORA unatekeleza ujenzi wa mitaro mikubwa ya maji ili kuondoa kero kwa wananchi hasa kipindi cha masika ambapo maji yamekuwa yakiingia kwenye makazi ya watu.
Akiongea wakati wa ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi mkoani hapa, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila ameitaka TARURA kuhakikisha mitaro hiyo inafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.
“Kuna haja ya kufanya matengenezo ya mara kwa mara na kufanya usafi katika mitaro hii ili maji yapite kwa urahisi na kuondoa kero kwa wananchi kama ilivyokusudiwa”.Amesema Mhandis Mativila.
Hata hivyo Mhandisi Mativila amewataka viongozi wa Manispaa na TARURA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi namna ya kutunza na kusafisha mitaro hiyo ili kuepuka mafuriko na magonjwa ya mlipuko.
Aidha,amewasihi wananchi wanaoishi karibu na mitaro hiyo kujitolea kwa hali na mali ili kuisafisha mitaro hiyo badala ya kukaa na kuisubiri serikali pekee.
Naye, Meneja wa TARURA Wilaya ya Tabora Mhandisi Subira Manyama amesema kuwa hadi sasa wamejenga mitaro yenye urefu mita 158 ambayo imesaidia wananchi kwa kiasi kikubwa.
“Kulikuwa na kero ya maji kuingia kwenye makazi ya watu lakini sasa kero hiyo imeondolewa ambapo mpango uliopo ni kuhakikisha tunaondoa kabisa mafuriko kwa kujenga mitaro yenye urefu wa km 25”.