Featured Kitaifa

WAZAZI WASHAURIWA KUWAFUNDISHA WATOTO UMUHIMU WA KUWEKA AKIBA

Written by mzalendo

Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro akitoa elimu ya fedha kuhusu Akiba na Bajeti kwa baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kipeta, Mkoa wa Rukwa Wilaya ya Sumbawanga Vijijini

Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro akiwafundisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Kipeta, iliyoko Mkoa wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini  kwa kuainisha vipengele muhimu kuhusu akiba.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kipeta, iliyoko Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, Mkoa wa Rukwa, wakijibu maswali kuhusu uwekaji, akiba na kupanga bajeti wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha linalofanywa na Wizara ya Fedha katika mikoa mbalimbali nchini.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha)

Na. Eva Ngowi, WF, Rukwa

Serikali kupitia Wizara ya Fedha imewashauri wazazi na walezi kuwafundisha Watoto kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba ili kuwasaidia katika Maisha yao ya baadae

Rai hiyo imetolewa na Afisa Mkuu Mwandamizi Idara ya Uendeshaji wa Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro wakati wa semina zinazoendelea katika miji na vijiji mkoani Rukwa, ikiwemo Shule ya Msingi Kipeta iliyopo Wilaya ya Sumbawanga Vijijini.

Bw. Kimaro alisema kuwa kuwafundisha Watoto kuweka akiba kutawajengea mfumo madhubuti wa kujenga uhakika wa masuala ya kifedha.

“Watoto wengi wamekiri kwamba walikuwa hawafahamu kwamba wanapopewa pesa wanatakiwa watumie kiasi na kiasi kingine waweke kama akiba ili siku wazazi wao wanapokosa pesa za kuwapa waweze kuzitumia.” Alisema Bw. Kimaro.

Bw. Kimaro alisema kuwa kwa sasa kuna taasisi mbalimbali kama vile Benki zinatoa elimu kwa Watoto kuhusu namna ya kuweka akiba, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walezi kutumia fursa hizo kwa ajili ya Watoto wao.

Awali akifundisha katika semina hiyo, Bw. Kimaro aliwataka wanafunzi hao wawe na tabia ama utamaduni wa kupanga bajeti na kwamba ili wapate akiba ya kuweka, inabidi hela wanayopewa na wazazi au iliyopangwa kununua vitu ipangiwe bajeti kwanza kwa vitu vilivyopangwa kunuliwa na itakayobaki iwekwe kama akiba.

Vilevile Bw. Kimaro alisema kuwa kuweka akiba ni njia za kuondokana na madeni yanayotokana na matumizi ya kila siku pamoja na gharama nyingine za maisha.

About the author

mzalendo