Featured Kitaifa

WAZIRI JAFO: MAPAMBANO DHIDI YA JANGWA YANAMGUSA KILAMMOJA

Written by mzalendo

 

Waziri wa Nchi Ofisi (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema mapambano dhidi ya ukame yanamgusa kila mmoja hivyo zinahitajika jitihada za pamoja kukabiliana na madhara yake.

Amesema kutokana na changamoto hiyo Serikali inatekeleza kwa vitendo mikakati mbalimbali ya kuhakikisha urejeshwaji wa ardhi na ustahimilivu wa hali ya ukame inayoyakabili baadhi ya maeneo nchini.

Dkt. Jafo amesema hayo wakati akishiriki kipindi cha Mizani kilichorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania kupitia Kituo cha Televisheni cha TBC1 tarehe 05 Juni, 2024, kuhusu Siku ya Mazingira Duniani yenye kaulimbiu ‘Urejeshwaji wa ardhi, Ustahimilivu wa Hali ya Jangwa na Ukame’.

Amesema kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wizara za kisekta inatekeleza miradi ya kimazingira katika maeneo mbalimbali nchini ambayo yanakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo mbali ya kusaidia katika mazingira lakini pia ina manufaa ya kiuchumi kwa wananchi.

Amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mapinduzi katika sekta kilimo ambayo inagusa moja kwa moja hifadhi ya mazingira kupitia kilimo cha kisasa.

“Tumeshuhudia bajeti ya kilimo imeongezeka ukilinganisha na miaka ya nyuma kwa mfano mifumo ya umwagiliaji imeboreshwa ambapo yanajengwa mabwawa ya umwagiliaji takriban 194 na hatua hii itasaidia sana wananchi katika maeneo yenye ukame kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji,” amesema Dkt. Jafo.

Ameongezeka kuwa katika kukabiliana na hali ya jangwa, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inaratibu zoezi la upandaji wa miti kwa halmashauri zote 184 nchini kwa lengo la kuwa na miti milioni 276.

Halikadhalika, Waziri Dkt. Jafo amebainisha kampeni ya ‘Soma na Mti’ inayowalenga wanafunzi wa kuanzia shule hadi vyuo ni chachu katika kuifanya nchi kuwa ya kijani na kukabiliana na hali ya ukame.

Hata hivyo, amesema baadhi ya shughuli za kibinadamu zinachangia katika uharibifu wa mazingira hivyo zipo jitihada za kuhakikisha kunakuwa na miongozo na kanuni za kudhibiti shughuli hizo.

Kutokana na hali hiyo amewapongeza washauri elekezi na wataalamu wa mazingira kwa kuendelea kufanya tathmni ya athari kwa mazingira kabla ya utekelezaji wa miradi pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kusimamia Sheria namba 191 ya Mazingira.

Amesema shughuli za kiuchumi lazima zifanyike lakini kila sekta inawajibika kulinda mazingira na kuwa uchimbaji wa mchanga au madini lazima uwe rafiki kwa mazingira kwa kuangalia athari zake ifanye jitihada za kulinda.

 

About the author

mzalendo