Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande, amewataka maafisa ununuzi wa taasisi za Serikali kuhakikisha wanatumia Mfumo wa Usimamizi wa Ununuzi wa Umma Kielektroniki (NeST) pekee kufanya ununuzi wa umma na kuhakikisha wanauelewa kuhusu moduli ya kuwasilisha malalamiko kupitia mfumo huo.
Maelekezo hayo ya Naibu Waziri ni msisitizo wa matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 itakayoanza kutumika rasmi Julai Mosi mwaka huu.
Chande ametoa maagizo hayo leo, Mei 29, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mafunzo ya moduli ya uwasilishaji wa malalamiko kupitia Mfumo wa NeST, yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa watumishi wa mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, na Pwani.
“PPAA kwa kushirikiana na PPRA hakikisheni kuwa mnatoa uelewa na mafunzo ya kutosha kuhusu moduli hii mpya ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya wazabuni kwa njia ya kielektroniki ili kuisaidia Serikali kupata thamani halisi ya fedha zinazotumika katika miradi mbalimbali,” amesema Naibu Waziri Chande.
Awali, Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando, alisema kuwa kuanza kutumika kwa moduli ya kupokea malalamiko kupitia Mfumo wa NeST kutaongeza ufanisi na kupunguza muda wa kushughulikia malalamiko. Alisema hatua hiyo pia imetokana na mabadiliko yaliyowekwa kwenye Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023.
Aidha, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Bi. Vicky Mollel, aliyemuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo na kuwasilisha mada kuhusu ujenzi wa Mfumo wa NeST, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuiwezesha mamlaka hiyo kujenga mfumo, na kwamba pamoja na moduli ya usajili, uendeshaji wa michakato na upokeaji wa malalamiko, inaendelea na ujenzi wa moduli ya mikataba (e-contract).
Aliwataka wazabuni na taasisi za Serikali kuendelea kuwasiliana na PPRA ili kupata huduma kwa haraka, ikiwa ni pamoja na kufika katika ofisi za Kanda ya Pwani zilizoko jengo la Hazina, jijini Dar es Salaam. Pia, wanapopata changamoto, wanaweza kuwasiliana na mamlaka hiyo kwa kutumia namba ya huduma kwa wateja ambayo ni 0736494948 na barua pepe support@nest.go.tz.