Featured Kitaifa

TANROADS YAWEKA KAMBI KUREJESHA MAWASILIANO BARABARA YA TINGI-KIPATIMO MKOANI LINDI

Written by mzalendo

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Lindi imeweka kambi ili kuhakikisha unarejesha mawasiliano katika barabara ya Tingi hadi Kipatimo wilayani Kilwa ambayo iliathiriwa na mvua za El-Nino na kimbunga Hidaya.

Kwa pamoja majanga hayo asili yalisababisha baadhi ya madaraja katika barabara hiyo kusombwa na maji jambo ambalo liliweka ugumu katika ufanyaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Akizungumza Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo amesema kambi hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Waziri wa ujenzi Mhe Innocent Bashungwa aliyetaka maeneo yote yaliyoathiriwa yapitike.

Eneo la kwanza lililokarabatiwa ni kujaza kifusi katika daraja lililokuwa limebebwa na maji lililopo katika kijiji cha Mingumbi ikiwa umbali wa kilomita 12.5 kutoka Tingi ilipo barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Mtwara.

Kujazwa kifusi katika eneo hilo la daraja sasa kutaruhusu ujenzi kuendelea katika maeneo mengine ya mbele hadi watakapomaliza.

Mhandisi msimamizi wa barabara hiyo, Fredy sanga amesema, awali barabara hiyo ilikuwa imeharibiwa kiasi na mvua za El-Nino lakini hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya Kimbunga Hidaya.

“Mvua zilizokuja na kimbunga Hidaya ilifanya barabara kukatika maeneo mbalimbali, daraja hili lililopo Mingumbi lilikatika na kusababisha njia hii kutopitika kabisa hivyo huduma kwa wananchi kuelekea kijiji cha Kipatimo kukosekana,” amesema Sanga.

Kwa upande wake Mkandarasi aliyepewa kazi ya kufanya marekebisho ya barabara hiyo, Kasmir Shirazi Mucadam ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mucadam and Sons limited amesema mvua ndiyo ilikuwa kikwazo katika utekelezaji majukumu yake.

“Tulisaini mkataba Machi mwaka huu lakini mvua ilikuwa changamoto, kwa sasaimetuachia tunapambana na kazi, madaraja mengi yalibebwa na maji hayapitikiti, tunatakiwa kujaza kifusi katika eneo moja baada ya lingine hadi tufike Kipatimo,” amesema.

Shamweji Mohamed ni Mtumiaji wa barabara ya Tingi-Kipatimo ambaye anafanya shughuli mbalimbali ikiwemo za kilimo, Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Ujenzi Mhe Innocent Bashungwa kwa kuhakikisha fedha zinapatikana ili kunusuru kadhia wanayokumbana nayo wananchi.

        

About the author

mzalendo