Na Gideon Gregory, Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande amesema Serikali inatambua na imeendelea kukumbusha kuwa Shilingi ndio fedha halali kwa ajili ya malipo mbalimbali hapa nchini ambapo kutokana na hilo, raia wa kigeni hawatakiwi kulazimishwa kulipa kwa fedha za kigeni hususani pale wanapokuwa na shilingi za kitanzania.
Naibu Waziri Chande ameyasema hayo leo Mei 20,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Dennis Londo Mbunge wa Mikumi aliyetaka kujua ni upi msingi kwa Wafanyabiashara kutoza bei tofauti au fedha za Kigeni kwa wateja ambao ni Raia wa Kigeni na nini athari zake.
Amesema wageni wanaruhusiwa kutumia fedha za kigeni ili kurahisisha ufanyaji wa biashara pale wanapokosa shilingi za Kitanzania na viwango vya ubadilishaji fedha haikitakiwi kutofautiana na vile vinavyotozwa katika masoko ya fedha.
“Hakuna athari zozote za kimsingi za uchumi (economic fundamentals) kwa wafanyabiashara kutoza bei tofauti baina ya wateja raia wa kigeni na wazawa kwani bei hizo huamuliwa katika soko huru na hivyo inatarajiwa kupanda na kushuka kulingana na nguvu za mahitaji na ugavi sokoni”,amesema.
Hata hivyo ameongeza kuwa wafanyabiashara wanaweza kutoza bei tofauti kwa bidhaa na huduma baina ya wazawa na raia wa kigeni au kwa fedha za kigeni.