Featured Kitaifa

TARI MAKUTOPORA YAZINDUA MKAKATI WA KUWANOA WAKULIMA WA ZABIBU DODOMA

Written by mzalendo

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kupitia kituo chake cha Makutupora jijjni Dodoma kinatekeleza programu maalumu ya kuwajengea uwezo wakulima wa zao la zabibu ili waweze kuzalisha kwa ubora na tija inayotakiwa.

Zabibu ni zao la kimkakati linalostawi vizuri mkoani Dodoma, lakini kwa miaka mingi sasa wakulima wanaojihusisha na uzalishaji wa zao hilo la kibiashara wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, hali ambayo imesababisha washindwe kuzisha kwa tija.

Changamoto husika ni ukosefu wa utaalamu wa kuandaa vitalu na miche bora, uandaaji wa mitaro na upandaji kwa vipimo vinavyopendekezwa kitaalamu, utunzaji wa mashamba ya zabibu, pamoja na uelewa mdogo juu ya aina ya viatilifu vya kupambana na visumbufu na magonjwa kwa ujumla.

Aidha, uelewa mdogo juu ya utaalamu wa ulimaji wa zao la zabibu miongoni mwa maafisa kilimo na maafisa ugani ni changamoto nyingine ambayo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya sekta ya uzalishaji wa zao la zabibu mkoani Dodoma.

Akizungumza wakati wa mafunzo maalumu kwa wakulima wa zabibu katika Wilaya ya Bahi, Dk. Lameck Makoye Nyaligwa, Mtafiti Mwandamizi wa kilimo kutoka TARI Makutupora amesema programu hiyo imejikita katika kuwajengea uwezo wakulima kukabilina na changamoto hizo.
“Program hii inalenga kuwafundisha wakulima mbinu bora zinazopendekezwa katika ulimaji wa zabibu, kuanzia hatua za awali za kuandaa vitalu na miche ya zabibu, jinsi ya kuchimba mitaro, na namna bora ya kuhamisha miche kutoka kwenye vitalu kwenda shambani,” alisema.

Maeneo mengine, amesema ni pamoja na jinsi ya kutunza zabibu zikiwa shambani, uwekaji wa mbolea na umwagiliaji, pamoja na kutambua matumizi sahihi ya viatilifu.

“Tunawafundisha namna ya kutambua viatilifu bora na viambata vyake ili waweze kukabilina na magonjwa na visumbufu vingine vya zabibu,” aliongeza.

Akiongoea baada ya kupatiwa mafunzo, Blandina Jarome, mkulima wa zabibu kutoka kata ya Mtitaa, kijijj cha Mtitaa, Wilaya ya Bahi, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mzuri wa kupambana na magonjwa ya zabibu.

“Tulikuwa tanapata shida sana katika kutambua dawa (viatilifu) sahihi, na hivyo mara nyingi tulikuwa tunapoteza pesa kwa kununua dawa ambazo hasitusaidii mashambani,”
“Mafunzo haya yamekuja kwa wakati sahihi na tunawaomba wataalam wa TARI wawe wanatutembelea na kutufundisha mara kwa mara,” alisema.

Kwa upande wake, Elias Thomasi, amesema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa wakulima kwani walikuwa wanalima zao hilo kwa mazoea tu bila kujua wala kufuata tannin za kitaalamu zinazotakiwa.

“Tumekuwa na jitihada sana za kulima zabibu lakini mara nyingi tunaishia kupata matokeo madogo shambani kinyume na matamanio. Lakini, kupitia mafunzo haya tumegundua tulikuwa na mapungufu mengi, kwa sasa tunashukuru kwa sababu wataamu wametujengea uwezo mzuri ambao utatuwezesha kuanza kulima kitaalamu na kwa tija,” alifafanua.

Afisa Kilimo kutoka halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Yusufu Shabani, ameiomba serikali kuangalia namna ya kuwawezesha wataalam hao kutoka TARI kuendesha mafunzo hayo mara kwa mara, kwa wakulima pamoja na maafika kilimo katika ngazi za kata na wilaya.

“Tumejifunza mengi kupitia mafunzo haya na tunatamani semina kama hizi ziwe zinafanyika mara nyingi ili kuwajengea wakulima ufahamu wa kitaalamu wa kulima zao hili kwa tija ” alipendekeza.

Katika wilaya ya Bahi, zao la zabibu linalimwa kwa wingi katika kata tatu za Mtitaa, Ibugure na Chibelela.

About the author

mzalendo