Featured Kitaifa

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA WANANCHI KUJENGA NA KUENDESHA HOSTELI

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba amesema mkakati wa serikali kupitia mamlaka za serikali za mitaa ni kuwashirikisha wananchi kujenga na kuendesha hosteli katika shule za kutwa za kidato cha kwanza hadi cha nne katika maeneo yenye uhitaji ili kutatua changamoto za ulinzi na usalama wa wanafunzi na kupunguza umbali wa kutoka nyumbani kwenda shuleni.

Mhe. Katimba ameyasema hayo leo Mei 10,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Neema Mwandabila Mbunge wa Viti Maalum aliyetaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kujenga Hostels katika Shule za Sekondari Nchini.

Amesema kwa sasa serikali imeweka kipaumbele cha ujenzi wa mabweni ya kidato cha tano na sita kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wote wanaofaulu kidato cha nne wanapata fursa ya kusoma elimu ya sekondari ya ngazi ya juu.

“Aidha, serikali itaendelea na jitihada zake za kuhamasisha wananchi kupitia mamlaka za serikali za mitaa kujenga na kuziendesha hosteli katika shule za sekondari za kidato cha kwanza hadi cha nne,”amesema.

About the author

mzalendo