Featured Kitaifa

WANANCHI 135,000 KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI MGULU WA NDEGE MOROGORO

Written by mzalendo

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew amesema Serikali inaendelea na ukamilishaji wa mradi wa maji Mgulu wa Ndege unaohusisha ujenzi wa kituo cha kusukuma maji (booster station), ujenzi wa matanki mawili yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 3 na mtandao wa mabomba ya usambazaji umbali wa kilometa 250.

Mhandisi Kundo ameeleza hayo leo Mei 10,2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Morogoro mjini Abdul-Aziz Abood aliyeuliza ni lini Serikali itamaliza Mradi wa Maji Tanki la Mgulu wa Ndege na kuanza kusambaza maji Kata za Mkundi, Kiegea na Kihonda Morogoro.

Mhandisi Kundo amesema hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 93 na baadhi ya wananchi wa Kata ya Kihonda wameanza kunufaika wakati utekelezaji ukiendelea kwa ajili ya kufikisha huduma kwenye Kata zilizobaki.

“Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2024 na wananchi wapatao 135,000 watanufaika na huduma ya majisafi kwenye Kata za Mkundi, Kiegea na Kihonda” amesema Kundo.

About the author

mzalendo