Featured Kitaifa

JENGO LA UTAWALA CHALINZE LIMECHOCHEA UTENDAJI KAZI NA UKUAJI WA UCHUMI – POSSI

Written by mzalendo

Na. James K. Mwanamyoto, OR-TAMISEMI

Jengo jipya la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze limechochea ari na morali ya utendaji kazi wa watumishi wa umma wa halmashauri hiyo pamoja na ukuaji wa shughuli za uchumi katika eneo linalozunguka jengo hilo.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze Bw. Ramadhani Possi alipofanya mahojiano na Afisa kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, alipomtembelea ofisini kwake kujua hali ya uwajibikaji wa watumishi mara baada ya kuanza kulitumia jengo hilo.

Bw. Possi amesema, jengo hilo la ghorofa tatu limekamilika kwa asilimia 100, lina lifti na uzio kwa ajili ya usalama wa watumishi na mali za ofisi na kuongeza kuwa limekuwa chachu ya kujenga ari na morali ya utendaji kazi wa watumishi pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika mji wa Chalinze.

“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutujengea jengo lililogharimu bilioni 5.7 ambalo limeamsha shughuli za kiuchumi na kuwawezesha watumishi wa idara zote kuwa na ofisi, na bado lina nafasi ya kutosha,” Bw. Possi amesisitiza.

Bw. Possi amefafanua kuwa, wananchi hivisasa wanafurahia huduma katika jengo jipya la utawala la Chalinze kwani zamani walikuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma Lugoba.

Kabla ya kukamilika kwa Jengo jipya la Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, ofisi za halmashauri hiyo zilikuwa Lugoba katika nyumba ambazo waliazimwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).

About the author

mzalendo