Featured Kitaifa

HAKUNA KAMPUNI YA SIMU INAYOTOA MIKOPO – DKT. MWIGULU

Written by mzalendo

Na Gideon Gregory,  Dodoma. 

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema hakuna kampuni ya simu inayotoa mikopo moja kwa moja, bali ni mabenki na taasisi za fedha zenye leseni kutoka Benki Kuu ndizo ambazo hutoa mikopo kupitia mifumo ya kampuni ya simu kwa makubaliano maalumu baina yao.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Mei 2,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum kutoka Kilimanjaro Mhe. Shally Reymond ni lini kampuni za simu zitalazimishwa kutoa elimu kwa wananchi kabla ya kutoa mikopo.

“Hata hivyo, Benki Kuu inafuatilia kwa karibu mwenendo wa utoaji wa mikopo ya kidigitali iliyoidhinishwa na pindi itakapobainika kuwa kuna ukiukwaji wa matakwa ya leseni ya utoaji wa mikopo hiyo, hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwafutia leseni. Benki Kuu imeshafuta baadhi ya leseni za mtoa huduma ndogo za fedha baada ya kubainika kampuni hizo zinatoa mikopo kinyume cha taratibu,”amesema.

Aidha ametoa rai kwa Benki Kuu ya Tanzania kuimarisha usimamizi wa sekta ya fedha hususani watoa huduma ndogo za fedha pamoja na watoa huduma za mifumo ya malipo kuhakikisha wanazingatia matakwa ya Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Sheria ya Mifumo ya Malipo ya mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2015.

Pua amewasihi wanachi wapate huduma za fedha kwa watoa huduma rasmi zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania ili kuepuka kutumia huduma za fedha kutoka kwa watoa huduma wasio rasmi na masharti magumu ikiwemo riba kubwa.

About the author

mzalendo