Featured Kitaifa

TANZANIA, MISRI YAENDELEZA MAKUBALIANO SEKTA YA AFYA

Written by mzalendoeditor

 

Na. WAF – Dodoma

Serikali ya Tanzania na Misri ziliingia mkataba wa makubaliano kati ya Wizara ya Afya na Shirika la ALAMEDA Healthcare Group Oktoba, 2022 ili kushirikiana katika nyanja ya Afya hasa upande wa huduma za kimatibabu kwa kubadilishana uzoefu, usimamizi wa hospitali na matibabu ya wagonjwa wa Kimataifa.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameeleza hayo leo Aprili 29, 2024 kwenye kikao chake cha kwanza na Balozi wa Misri nchini Tanzania Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail kilichofanyika katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma.

“Ni furaha kwetu kuendelea kushirikiana katika kubadilishana wataalamu wa Afya, kubadilishana teknolojia na programu za mafunzo na elimu, kubadilishana madaktari, wauguzi, mafundi wa radiolojia, mafundi maabara pamoja na wanasayansi wa tiba.” Amesema Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amemuomba Balozi huyo kusaidia wahudumu wa Afya ya Jamii (CHWs) watakao ajiriwa 137,000 wenye jukumu muhimu la kutoa huduma za Afya kwa watu ambao hawajafikiwa.

“Chini ya utaratibu huu, itaashiria uwekezaji mkubwa wa rasilimali watu na uwezeshaji wa jamii ili kufikia lengo hili, ushirikiano ni muhimu kuweza kukusanya rasilimali kutoka kwa washirika na kutumia miundombinu na mitandao iliyopo.” Amesema Waziri Ummy

Kwa upande wake Balozi za Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Nchini Tanzania Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail amemshukuru Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kumkaribisha na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo Mbili.

About the author

mzalendoeditor