Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Mhe. Usekelege Nahshon Mpulla, amewataka wananchi kuhakikisha wanawasilisha migogoro ya kikazi kwa wakati ndani ya Tume badala ya kuzipeleka kwa wakuu wa wilaya na sehemu zisizohusika.
Ametoa wito huo leo Aprili 25,2024 wakati akifanya mahojiano katika ofisi za makao makuu ya Tume jijini Dodoma.
Mkurugenzi amesema pale wananchi wanapokua na changamoto za migogoro ya kikazi na kuipeleka katika ofisi za wakuu wa wilaya na mahali pengine tofauti na Tume ni sababu mojawapo inayopelekea kuchelewa kufungua migogoro ndani ya Tume.
Aidha, Mpulla amesema elimu kuhusu migogoro ya kikazi imesaidia pia kupunguza idadi ya migogoro inayosajiliwa Tume kutokana na idadi ya migogoro kupungua kutoka idadi ya migogoro 17,963 iliyosajiliwa kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi kufikia migogoro 11,759 kwa mwaka 2022/2023 na kupungua hadi kufikia idadi ya migogoro 4,579 ambayo ni hadi February 2024.
Ameongeza kuwa, lengo la Tume ni kuhakikisha inaokoa muda kwa kuwasaidia wadaaawa kupata suluhu ya migogoro yao ili kuweza kuokoa muda kwani usuluhishi ndio njia bora zaidi katika utatuzi wa migogoro ya kikazi na kuwasaidia wadaawa kuendelea na shughuli za kimaendeleo.
Vilevile ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kusaidia Tume kuhakikisha wanafanikisha shughuli mbaalimbali za Tume zilizopelekea kuboresha huduma na kupunguza migogoro ya kikazi.
Akitoa shukrani hizo ameongeza kuwa Tume imepata fedha kwaajili ya kusimika mfumo wa kusajili mashauri na ambao utawezesha watanzania na watu wote wenye changamoto ya migogoro mahala pa kazi kujisajili kokote waliko ikiwa na lengo la kupunguza gharama ya kufuata ofisi za Tume kwaajili ya kufungua migiogoro.
Aidha, Mpulla amesema mfumo mpya wa kusajili mashauri unaoendelea kusimikwa maeneo mbalimbali nchini katika ofisi za Tume, utasaidia pia katika kuhakikisha wadau mbalimbali wenye migogoro ya kikazi kufungua migogoro kwa wakati kwa muda uliolekezwa kisheria kwa lengo la kupunguza changamoto za kuwasilisha madai Tume baada ya muda kupita.
Vilevile amewataka waajiri na waajiriwa kutumia njia ya usuluhishi ili kuweza kuokoa muda na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali na maendeleo kwani ndio njia bora katika utatuzi wa migogoro ya kikazi na yenye faida nyingi kulinganisha na njia ya uamuzi.