Featured Kitaifa

IMF NA EAC WAJADILI UKUSANYAJI MAPATO YA NDANI KWA AJILI YA MAENDELEO

Written by mzalendo
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza katika mkutano uliotishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF na kuwakutanisha Wadau kutoka nchi za Afrika Mashariki, wakati wa mikutano ya Kipupwe (Spring Meetings), jijini Washington D.C nchini Marekani, ambapo walijadili namna nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinavyoweza kujitegemea kwa kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kutemea mikopo na misaada kutoka nje.
Mkutano ulioitishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF ukiendelea, wakati wa mikutano ya Kipupwe (Spring Meetings), jijini Washington D.C nchini Marekani, ambapo wadau walijadili namna nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinavyoweza kujitegemea kwa kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kutemea mikopo na misaada kutoka nje.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (kulia) na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, wakifuatilia mkutano uliotishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, wakati wa mikutano ya Kipupwe (Spring Meetings), jijini Washington D.C nchini Marekani, ambapo wadau walijadili namna Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinavyoweza kujitegemea kwa kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kutemea mikopo na misaada kutoka nje. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,WF,Washington).
………..
Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amezishauri nchi za Afrika Mashariki kuunganisha nguvu na kuweka mikakati thabiti ya pamoja ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukuza uchumi na huduma za jamii.
Dkt. Mwamba ametoa rai hiyo, wakati akizungumza katika mkutano uliotishwa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, wakati wa mikutano ya Kipupwe (Spring Meetings), jijini Washington D.C nchini Marekani, ambapo wadau walijadili namna nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinavyoweza kujitegemea kwa kuboresha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kutemea mikopo na misaada kutoka nje.
Alisema kuwa nchi za Afrika Mashariki, kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea duniani, zinafanya kila jitihada ya kutekeleza Bajeti zao kwa kutumia mapato ya ndani na kuwekeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo bila kutegemea kwa kiwango kikubwa mikopo kutoka nje ya nchi.
Dkt. Mwamba alieleza kuwa pamoja na jitihada hizo, bado nchi hizo za Afrika Mashariki zinapata changamoto ya kufikia malengo husika ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambapo uwiano wa mapato yatokanayo na kodi na pato la Taifa kwa nchi katika mwaka 2023 ulikuwa asilimia 13.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 16.5 katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Alizitaja baadhi ya hatua ambazo Tanzania inazichukua katika kuboresha ukusanyaji mapato ya ndani, ya kodi na yasiyo ya kodi kuwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri yanayovutia uwekezaji wa mitaji kutoka ndani na nje ya nchi, kuweka mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji mapato na kurasimisha biashara ya sekta isiyorasmi.
Dkt. Mwamba alielezea pia umuhimu wa wananchi kuelimishwa kuhusu faida za kulipa kodi kwa manufaa ya maendeleo yao halikadhalika wananchi wanatakiwa waone miradi inayotekelezwa kwa ajili ya maendeleo yao ikiwemo elimu, afya, miundombinu, maji, nishati na mambo mengine, haiwezi kufikiwa bila wao kulipa kodi kikamilifu. 

About the author

mzalendo