Featured Kitaifa

ZBC YAWANYANYUA WAJASIRIAMALI WAKIADHIMISHA MIAKA 11 TANGU KUANZISHWA KWA SHIRIKISHO HILO

Written by mzalendo

Waziri wa Habari, Vijana , Utamadini na Michezo Mhe. Tabia Maulid Mwita akizungumza na watendaji wa Shirika la utangazaji Zanzibar ZBC katika sherehe ya kutimiza miaka kumi na moja (11) tokea kuanzishwa kwake, hafla ambayo imefanyika Karume house Mjini Unguja.

Waziri wa maendeleo ya Jamii,Jinsia Wazee na Watoto  Mhe. Riziki Pembe Juma akizungumza na watendaji wa Shirika la utangazaji ZBC wakati wa sherehe ya kutimiza miaka kumi na moja (11) tokea kuanzishwa kwa shirika hilo huko Karume house Mnazimmoja Wilaya ya Mjini. (PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR.)

Na Fauzia Mussa Maelezo.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe.Tabia Maulid Mwita amesema Shirika la utangazaji Zanzibar ZBC litasaidia wajasiriamali wenye ulemavu kutangaza kazi zao bila malipo kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kupeleka mrejesho kwa jamii.

Akizungungumza na wajasiriamali hao huko  Karume house katika kusherehekea kutimiza miaka 11 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo  amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi kuona shirika hilo linachangia na kuisaidia jamii hasa wanawake na wenye ulemavu.

Amesema wajasiriamali 11 kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba wamependekezwa na Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais kupitia Baraza la Taifa la Watu wenye ulemavu Zanzibar kupata fursa hiyo  na kuahidi kuongeza idadi zaidi kwa kila mwaka.

Aidha Waziri Tabia ameahidi kuwaunganisha wajasiriamali hao na masoko mbali mbali ili kuweza kuuza bidhaa zao na kujipatia kipato, kitakachoweza kusaidia kuendesha Maisha yao ya kila siku.

Sambamba na hayo amewataka watendaji wa washirika hilo, kuendelea kufanya kazi kwa bidii, mashirikiano na umoja ili kuendeleza mafanikio waliyoyapata na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizopo ili kuimarisha utendaji.

Hata hivyo Waziri Tabia amemkumbusha Mkurugenzi wa shirika hilo kuwakumbuka viongozi waliowahi kuliongoza shirika  hlyo kwani wametoa njia na miongozo iliopelekea kutoka Tvz/Stz hadi kuwa ZBC.

 Kwa upande wake Waziri wa maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amelipongeza shirika hilo kwa kutimiza miaka 11 sambamba na kuwasaidia Wajasiriamali 11 wenye ulemavu hasa Wanawake jambo ambalo linatimiza malengo ya Serikali katika kuwafikia watu hao kwa ukaribu zaidi.

Amefahamisha kuwa jukumu la kuisaidia jamii hasa kumnyanyua Mwanamke sio la Wizara ya maendeleo ya Jamii pekee bali ni la kila mtu kulingana na nafasi alionayo.

“Kitendo hicho walichokifanya ZBC ni cha kupongezwa kwani kimegusa moja kwa moja majukumu ya wizara hii kwani tunaona watu wenye ulemavu wameachwa nyuma kwa muda mkubwa” alisema Waziri Pembe.

Amesema ubunifu huo uliofanywa na ZBC, umeonyesha kupiga hatua za maendeleo na kuongeza mafanikio katika shirika hilo sambamba na kuziomba taasisi nyengine kuiga mfano huo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar ZBC Ramadhan Athuman Bukini amesema mafanikio yaliopatikana katika shirika hilo yanatokana na juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi za kuliunga mkono shirika hilo kupitia Wizara ya habari, hivyo wameahidi kuendelea kuwa bega kwa bega na kiongozi huyo katika kuwasaidia wananchi. 

Miongoni mwa Wajasiriamali hao akiwemo Khamis Makame kutoka Mkoa wa kaskazini Unguja na Fatma zahor kutoka Mkoa wa Mjini Magharaibi wameiomba Serikali kuwajengea maeneo maalum ya biashara  wajasiriamali wenye ulemavu ili kuondoa usumbufu sambamba na kuushukuru uongozi wa ZBC kwa kuwapatia fursa hiyo.

Shirika la utangazaji Zanzibar ZBC lilianzishwa April 29, 2013 baada ya kuunganishwa iliokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ) na Televisheni ya Zanzibar (TVZ).

About the author

mzalendo