Featured Kitaifa

MHE.KATIMBA : BARABARA ZA LAMI KM 102 KUJENGWA MBOGWE

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Serikali inatarajia kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa RISE katika Wilaya ya Mbogwe zenye jumla ya urefu wa kilomita 102.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais- TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba ameyasema hayo leo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe Mhe. Nicodemas Maganga ambaye ametaka kujua lini barabara za lami zinazofadhiliwa na Benki ya Dunia zitaanza kujengwa Mbogwe.

Katimba akijibu swali hilo, amezitaja barabara zitakazojengwa kwenye mradi huo kuwa ni Masumbwe – Iponya – Nyashimba (km 20), Lulembela – Kiseke – Isebya (km 17), Mkweni – Nhomolwa – Nyanhwiga (km 21), Ishigamva – Busabaga – Ilolangulu (km 14) na Ivumwa – Ushirika – Shibutwe (km 30).

“Utekelezaji wa mradi huu utafanyika kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa barabara za Masumbwe – Iponya – Nyashimba (km 20.0), Lulembela – Kiseke – Isebya (km 17.0), Ishigamva – Busabaga – Ilolangulu (km 14.0) na Mkweni – Nhomolwa – Nyanhwiga (km 21.0). “

“Aidha, kazi za usanifu wa barabara za awamu ya kwanza zilianza Januari, 2024 na zinatarajiwa kukamilika Agosti, 2024 baada ya kazi ya usanifu wa Barabara kukamilika, Serikali kupitia TARURA itatangaza Zabuni na kumpata Mkandarasi wa kujenga Barabara za awamu ya kwanza kwa kiwango cha lami,” amesema.

&&&&

About the author

mzalendo