Featured Kitaifa

VIJIJI 40 IRAMBA KUANDALIWA MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI

Written by mzalendoeditor

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Bw. Suleiman Mwenda akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 17 Aprili 2024 katika Wilaya ya Iramba, Singida
Na. Magreth Lyimo, MLHHSD
Vijiji takribani 40 katika Wilaya ya Iramba Mkoani Singida vitanufaika na Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Iramba Bw. Suleiman Mwenda wakati wa kufungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi huo katika ukumbi wa Halmashauri ya Iramba, tarehe 17 Aprili 2024 Mkoani Singida.

Alisema mpaka sasa mradi wa LTIP umefanikiwa kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 20 ikiwa lengo ni kufikia vijiji 40 katika Wilaya hiyo ambapo utekelezaji wa mpango huu utaleta matokeo chanya katika kuchochea maendeleo, kuongeza usalama wa milki za ardhi, kukuza huduma za kiuchumi na kijamii, kuboresha hifadhi ya mazingira na kumaliza migogoro itokanayo na ardhi.

Mwenda alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huo katika Wilaya ya Iramba utakaosaidia kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya Vijiji yatakayoainisha matumizi mbalimbali ya kijamii kulingana na uhitaji wa Kijiji husika.
Aidha aliwataka Waheshimiwa Madiwani, Watendaji wa Kata na Vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha utekelezaji wa Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji katika Wilaya hiyo.

Nae Meneja Mradi Msaidizi Urasimishaji Vijiji Bw. Patrick Mwakilili amesema kuwa mradi una lengo la kuboresha usalama wa milki za ardhi kwa kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinatambuliwa, kinapangwa, kinapimwa na kumilikishwa.

‘‘Mradi huu katika hatua zote umeweka nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi kuanzia ngazi ya Kitaifa, Wilaya, Mtaa/Kijiji mpaka Kitongoji ikiwa ni pamoja na kuzingatia haki za makundi mbalimbali yakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wanawake, vijana, wenye ulemavu sambamba na utoaji wa elimu ya usawa wa jinsia katika umiliki wa Ardhi ili kuhakikisha usalama kwa kila kipande cha ardhi kwa Mtanzania’’ alisema Mwakilili

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umedhamiria kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji takribani 1667 katika Halmashauri zisizopungua 30 nchini.


Mkuu wa Wilaya ya Iramba Bw. Suleiman Mwenda akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 17 Aprili 2024 katika Wilaya ya Iramba, Singida


Wadau walioshiriki katika Mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 17 Aprili 2024 katika Wilaya ya Iramba, Singida

Meneja Mradi Msaidizi wa Urasimishaji Vijiji Bw. Patrick Mwakilili akitoa taarifa fupi ya utekelezaji mradi wa uboreshaji wa usalama wa miliki za ardhi tarehe 17 Aprili 2024 katika Wilaya ya Iramba, Singida

About the author

mzalendoeditor