Featured Kitaifa

KINANA ASHAURI WATUMISHI, WATAALAMU SERIKALINI WASITOE AHADI BILA MIPANGO

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Mara.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana ameeleza kuwa, ni vema Watumishi, wataalamu wa serikali kutotoa ahadi ambazo wanajua hazitatekelezeka au utekelezaji wake utachukua muda mrefu kukamilika kwani imekuwa ikikwamisha shughuli za maendeleo na kusababisha malalamiko kwa wananchi.

Kinana meeleza hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Bunda Mjini wilayani Bunda mkoani Mara baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kuwa serikali imewataka wahame katika maeneo yao kupisha ujenzi wa mradi wa maendeleo.

Pia, wananchi hao walionesha kukerwa na kitendo cha maeneo yao kuchukuliwa, nyumba kubomolewa na kupewa sharti la kutoendeleza maeneo hayo likiwemo eneo la Kijiji cha Nyantwale.

“Viongozi wa serikali kabla ya kuwahamisha wananchi ni vema wakaeleza ni lini ahadi hiyo itatekelezwa, kama ni fidia, lini fidia hiyo itatolewa, kama ni watu kuhama watahama lini, kama watu ni kupewa fidia watapewa lini,” amesema.

Aliongeza kuwa, hakuna sababu ya kutoa ahadi ambayo inachukua miaka mingi kutekelezwa na kila kiongozi anayekuja anatoa ahadi anaondoka.

Kinana alishauri watendaji wa serikali kabla ya kufanya uamuzi unaohusu kuhamisha watu, kufidia au kufanya jambo lolote linalohusu wananchi, ni vyema wafanye utafiti wa kutosha kupata uhakika kuhusu malipo ya wananchi, fedha zipatikanaje ndipo watoe kauli, na si vyema kauli itangulie kabla ya kutanguliza fidia.

Makamu Mwenyekiti Kinana alisema kuwa, kumekuwapo na tabia ya kuwaeleza wananchi kuhusu kuhama au kutohama halafu hakuna kinachoendelea.

Kinana alifafanua zaidia kwa kueleza kwamba, “viongozi na watendaji acheni utaratibu wa kutoa ahadi bila ya kujiandaa, ni muhimu mkajipanga kwanza ili mnapotoka na majibu muwe na uhakika na mnachosema.”

About the author

mzalendo