Featured Kitaifa

VIPAUMBELE VYA TAMISEMI HIVI HAPA KWA MWAKA 2024-2025

Written by mzalendo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza wakati wa kuwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zake kwa mwaka 2024/25.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Adolf H. Ndunguru akiwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (TAMISEMI), Sospeter M. Mtwale, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Dkt. Charles Msonde, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) Dkt. Wilson Mahera na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI (Miundombinu) Mhandisi Rogatus Mativila wakifuatilia uwasilishwaji Bungeni wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, Bungeni jijini Dodoma. Leo Aprili 16, 2024.
  Wakuu wa Mikoa Tanzania Bara wakimfuatilia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) akiwasilisha Bungeni Makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa mwaka wa fedha 2024/25, Bungeni jijini Dodoma. Leo Aprili 16, 2024.
Na Alex Sonna,Dodoma 
OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetaja vipaumbele vya  bajeti kwa mwaka 2024-2025 ikiwemo kusimamia Uchaguzi wa Serikali za mitaa ambapo imetenga zaidi ya Sh bilioni 17 kwa ajili ya kugharamia Uchaguzi huo.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 17,2024 bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Tamisemi,Mohammed Mchengerwa wakati akiwasilisha makadirio na mapato ya Ofisi hiyo kwa mwaka 2024-2025.
Waziri Mchengerwa amesema  Ofisi ya Rais – TAMISEMI imetenga shilingi bilioni 17.79 kwa ajili ya kuratibu na  kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa  Mwaka 2024. 
Amesema kati ya fedha hizo shilingi bilioni 8.00 ni fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya uratibu Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Makao Makuu) na  shilingi bilioni 9.79 ni mchango wa halmashauri kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huo. 
“Uchaguzi huu utahusu uchaguzi wa  viongozi katika ngazi ya msingi ambao ni wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji, wajumbe wa halmashauri ya vijiji,”amesema Waziri Mchengerwa
VIPAUMBELE
Amevitaja vipaumbele vya Ofisi hiyo ni  Kusimamia shughuli za utawala bora,kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa  wananchi na ugatuaji wa madaraka kwa  umma (D by D).
Pia,Kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma za jamii.
Vilevile Kuratibu na kusimamia mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na  kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika  ngazi zote ikijumuisha kuongeza kasi ya  biashara ya kaboni.
Pia,Kuratibu na kusimamia mifumo na miundombinu ya TEHAMA,Kuendeleza rasilimaliwatu katika ngazi  zote za Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Amevitaja vipaumbele vingine ni kuratibu na kusimamia shughuli za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.
 BILIONI 500 KWA AJILI YA MAENDELEO
Waziri Mchengerwa amesema Ofisi yake  imepanga kutumia shilingi bilioni 541.27 za mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuchangia utekelezaji  wa shughuli za maendeleo.
Amezitaja shughuli hizo ni pamoja na  ujenzi na ukamilishaji wa vituo vya afya 132,zahanati 289, hospitali 21, vichomea taka 26, majengo ya wagonjwa wa nje 14, wodi 41, majengo ya kufulia matatu (3), majengo yakuhifadhia maiti nane (8), njia za kupita wagonjwa kwenye vituo vinne (4) vya kutolea  huduma za afya.
Pia,maduka mawili ya dawana ununuzi wa vifaa tiba katika vituo nane (8) vya kutolea huduma.
Pia ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa vyumba vya madarasa 2,871, maabara za masomo ya sayansi 203 za sekondari, shule za msingi na sekondari 88, matundu ya vyoo 5,730 vya wanafunzi na walimu, mabweni 88, hosteli 24, mabwalo 19, majiko mawili (2), maktaba  6 na ofisi za walimu 48.
Aidha, ununuzi wa madawati 47,192 katika shule za msingi, viti na meza 40,585 pamoja na vitanda 60.
Pia,Ujenzi wa uzio katika majengo 42 ya umma,ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilometa 8.4 kwa  kiwango cha lami.
Vilevile kufanya matengenezo ya kawaida na kufungua barabara kuelekea  maeneo ya uzalishaji.
Vilevile Uwekezaji na utoaji wa  huduma, kuchangia ujenzi wa barabara za  mijini na vijijini kupitia TARURA na ujenzi wa vivuko vinne (4) vya watembea kwa miguu.
VIPAUMBELE OFISI ZA WAKUU WA MIKOA
Waziri Mchengerwa amesema  ofisi za wakuu wa mikoa zinatarajia kutekeleza vipaumbele mbalimbali ikiwemo Usimamizi wa masuala ya usalama, Uratibu wa maandalizi na uchaguzi wa  serikali za mitaa wa mwaka 2024.
Pia,Uimarishaji wa utawala bora, uwajibikaji na uwazi kwa kufanya vikao vyote vya kisheria,Uratibu na usimamizi wa utoaji wa huduma za jamii,uratibu wa uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Vilevile, Kudhibiti matumizi yasiyo na tija,Uboreshaji wa mazingira ya kufanyia kazi na makazi ya viongozi na watumishi wa mikoa na wilaya.
MKAKATI WA UKUSANYAJI MAPATO
Mchengerwa amesema  katika kuhakikisha kuwa mapato ya mamlaka za serikali za mitaa yanakusanywa kwa ufanisi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI itaendelea  kufanya tathmini juu ya ukusanyaji wa mapato na kuendelea kubuni vyanzo vipya ili kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Vilevile kuendelea na zoezi la kuratibu uthamini  wa majengo ili kuweza kutoza kodi ya majengo kwa kutumia thamani halisi ya jengo husika.
” Kuendelea kuimarisha Mfumo wa TAUSI ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kwa yeyote atakayebainika kuhusika na upotevu wa  mapato.
“Kuendelea kuimarisha upatikanaji wa  vifaa vya kukusanyia mapato ikiwemo  ununuzi wa PoS,”amesema Waziri Mchengerwa.
MIKOPO YA ASILIMIA 10
Waziri Mchengerwa amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeendelea kuzisimamia mamlaka za serikali za mitaa kutenga fedha kwa ajili ya mikopo itokanayo na asilimia 10  ya mapato ya ndani ya halmashauri yasiyolindwa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. 
Amesema tangu mikopo hiyo ilipositishwa MweziAprili, 2023 hadi Machi, 2024 fedha iliyopo kwenye 
akaunti za halmashauri ni shilingi bilioni 63.24. 
Aidha, fedha za marejesho ya mikopo zilizopo kwenye akaunti husika kwa kipindi hicho ni shilingi bilioni 63.67.
USIMAMIZI NA UENDESHAJI ELIMU MSINGI NA SEKONDARI
Amesema Ofisi ya Rais – TAMISEMI imepanga kutumia shilingi trilioni 1.02 kupitia ruzuku ya serikali kuu na washirika wa maendeleo kwa ajili  ya utekelezaji wa shughuli katika sekta ya elimu.
Amesema wamepanga Ujenzi wa vyumba vya madarasa 6,357, matundu ya vyoo 1,482, umaliziaji wa 
mabwalo 362 kati ya mabwalo hayo 15 ni msingi na 347 ni ya sekondari na  umaliziaji mabweni 36 kwenye shule za  awali na msingi.
Pia ujenzi wa shule mpya 184, nyumba za walimu 184 na mabweni 186 katika shule za sekondari,ununuzi wa vifaa vya TEHAMA kwenye  shule za awali 3, msingi 400 na shule za 
sekondari 500.
Pia, Ununuzi wa kemikali za maabara katika shule mpya 234, Utoaji wa ruzuku ya Elimu Bila Ada kwa shule za msingi 17,986 na sekondari 4,894.
Vilevile Ununuzi na usambazaji wa vitabu 2,215,877 kwa shule za msingi na 11,880,828 kwa shule za sekondari pamoja na vitabu na vifaa vilivyoboreshwa vya kufundishia na  kujifunzia elimu ya awali kwenye shule  4,500.
Pia,Ununuzi wa vifaa saidizi kwa wanafunzi  wenye mahitaji maalumu katika shule 130 za msingi na sekondari.
Mwisho

About the author

mzalendo