Featured Kitaifa

SERIKALI KUENDELEZA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA NA MAAMBUKIZI YA UKIMWI

Written by mzalendo

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Serikali imesema imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini hatua itakayosaidia kunusuru kundi kubwa la vijana ambao wamekuwa waathirika wakubwa wa dawa hizo.

Kauli hiyo imetolewa Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati akitoa ufafanuzi wa michango ya waheshimiwa wabunge katika kuhitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi hiyo pamoja na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Mhe. Mhagama alisema serikali imefanikiwa katika hatua mbalimbali za mapambano hayo zikiwemo kuongezeka kwa waraibu kujitokeza kupata huduma katika Vituo tiba visaidizi vinavyojulikana kama Medication Assited Therapy Clinics (MAT CLINICS), kukamatwa kwa kemikali bashirifu kilo 22,143 , ukamataji wa dawa za kulevya ambapo kwa mwaka 2023 Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawaza Kulevya Tanzania (DCEA) ilikamata kilo milioni 1.8 za dawa mbalimbali.

“Kiwango hicho kilichokamatwa ni mara tatu ya ukamataji ambao umefanyika kwa kipindi cha miaka 11 yote haya ni kwa sababu ya utashi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mapamabano ya matumizi ya dawa za kulevya, tumeboresha sheria. Pia Mheshimiwa Rais ametoa fedha za kununua vitendea kazi kama boti ya kufanya kazi katika Bahari Kuu, mafunzo kwa wataalam na uzalendo wa watumishi wa mamlaka hii,”Alibainisha Mhe. Mhagama.

Vilvile amesema kwamba lengo la kuongeza juhudi katika mapambano ya dawa za kulevya ni kuokoa nguvu kazi ya Taifa kwani kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi vijana wenye umri wa miaka 15-35 ni zaidi ya milioni 20 hivyo ipo haja ya kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya .

“Mpaka sasa tuna vituo visaidizi vya tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya kutoka 11 mpaka 16 na tumepiga sana kama Nchi kwani takribani waraibu 16,000 wameanza kujitokeza katika vituo vya kupata tiba hii inamaanisha mtaani dawa za kulevya zimepungua hivyo hatuna budi kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya,”Alipongeza.

Kwa wakati tofauti akijibu hoja za wabunge kuhusu masuala ya UKIMWI Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga alieleza kwamba Serikali kwa kushirikiana na Wadau inatekeleza Awamu ya pili ya Programu ya Wasichana Balehe na Wanawake Vijana ya mwaka 2024 – 2026 itakayohusisha Wavulana Balehe na Wanaume Vijana ambapo wote watapatiwa huduma jumuishi za Kitabibu, Kitabia na Kimfumo pamoja na elimu ya Ujasiriamali kwa walengwa.

“Serikali kwa kushirikiana na Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA) imeunda vikundi vya WAVIU chini ya Konga katika kila Halmashauri ambao hunufaika na mikopo ya Halmashauri ya 4-4-2. Aidha, Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) umetenga 10% ya fedha za Mfuko kwa ajili ya kuwawezesha WAVIU kiuchumi,”Alieleza Mhe. Nderiananga.

Aidha Mhe. Nderiananga alifafanua kwamba Baraza la Taifa la kuwezesha wananchi kiuchumi (NEEC) limeingia makubaliano (MoU) na PPRA kuhusu utekelezaji wa mpango kabambe wa kushirikisha makundi maalum ya wanawake, Vijana, Wazee na wenye ulemavu kuinua uchumi wao kupitia Manunuzi ya Umma kwa kiasi cha 30%. 

About the author

mzalendo