Featured Kitaifa

MHE.KAPINGA ATEMBELEA WIKI YA NISHATI 2024 BUNGENI DODOMA

Written by mzalendo

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akizungumza na Wataalam mbalimbali kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati walioshiriki Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akiangalia utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere kupitia kifaa cha uhalisia pepe (VR) katika Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga akipata maelezo kuhusu utekelezaji wa Sekta ya Nishati katika Wiki ya Maonesho ya Nishati inayoendelea katika Viwanja  vya Bunge jijini Dodoma. Anayetoa maelezo ni mtaalam kutoka Wizara ya Nishati Joyce Msangi.

……

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ametoa wito kwa wananchi na Wabunge nchini kutembelea Maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma ili kufahamu masuala mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali chini ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Naibu Waziri Kapinga ametoa wito huo tarehe 15 Aprili, 2024  baada ya kutembelea mabanda ya Maonesho hayo na kujionea jinsi Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Wadau wake walivyojipanga tayari kwa kuhudumia Wabunge na Wananchi watakaotembelea maonesho husika.

“ Nawakaribisha Wananchi na Wabunge kwenye Wiki hii muhimu sana ya Nishati, ambapo tunaonesha kazi mbalimbali zinazofanywa na Wizara ya Nishati pamoja na Taasisi zake, tunatatua kero mbalimbali zinazowasilishwa na pia Wabunge na Wananchi watajionea utekelezaji wa miradi katika wilaya zote, majimbo yote na mikoa yote Tanzania.”amesema Mhe. Kapinga

Ameongeza kuwa, katika Maonesho hayo Taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na kampuni zake tanzu zimeshiriki.

Mhe. Kapinga amesema kuwa, katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kazi kubwa imefanyika katika Sekta ya Nishati akitolea mfano utekelezaji wa miradi mbalimbali ukiwemo wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao umeshaanza kuzalisha umeme, miradi ya usambazaji umeme mijini, vijijini na vitongojini, nishati safi ya kupikia pamoja
na sekta ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia.

Aidha, kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,  Mhe. Kapinga amemshukuru Spika wa Bunge, Mhe. Dkt.Tulia Ackson kwa kutoa ushirikiano kwa Wizara ya Nishati ambao umewezesha Wiki ya Nishati kufanyika kwa umahiri mkubwa.

Maonesho ya Wiki ya Nishati yaliyoanza leo yatahitimishwa tarehe 19 Aprili 2024 ambapo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko atayafungua rasmi tarehe 16 Aprili 2024.

About the author

mzalendo