Featured Kitaifa

VIJIJI 60 NKASI KUNUFAIKA NA MRADI WA LTIP

Written by mzalendo

 

Akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Lazaro Komba akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 08 Aprili 2024 katika Wilaya ya Nkasi, Rukwa.

Wadau walioshiriki katika Mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi tarehe 08 Aprili 2024 katika Wilaya ya Nkasi, Rukwa.

Meneja Mradi Msaidizi wa Urasimishaji Vijiji Bw. Patrick Mwakilili akitoa taarifa fupi ya utekelezaji mradi wa uboreshaji wa usalama wa miliki za ardhi tarehe 08 Aprili 2024, katika kikao cha wadau Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa.

Na. Magreth Lyimo, MLHHSD

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) imeendelea kuhakikisha inaongeza thamani katika ardhi za Watanzania ambapo katika Wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa takribani vijiji 60 vitanufaika na mradi huo kwa kupangiwa matumizi ya ardhi ambapo mpaka sasa vijiji 45 matumizi yake yamekwishaandaliwa.

Akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mhe. Lazaro Komba alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano wa wadau kujadili utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika ukumbi wa Ngunga, tarehe 08 Aprili 2024 Mkoani Rukwa.

Alisema mbali na mradi wa LTIP kupanga matumizi ya ardhi ya vijiji wilayani humo, mradi umefanikiwa kuhamasisha wananchi takribani 23,220 kuhusu ushiriki wao katika zoezi la uandaaji wa matumizi ya ardhi, jumla ya vyeti vya vijiji 30 tayari vimeandaliwa na vingine 15 viko katika hatua za mwisho ambapo uandaaji wa vyeti hivi utatoa hadhi kwa Halmashauri ya Kijiji kuwa na Mamlaka ya kusimamia Ardhi ya Kijiji husika kwa mujibu wa Sheria.

Alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi huo wilayani Nkasi kwa kuwa utayarishaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Vijiji umetoa fursa ya kipekee ya kumaliza changamoto zinazohusiana na matumizi ya Ardhi kama vile migogoro ya mipaka, migongano ya matumizi ya ardhi, uharibifu wa mazingira na ukosefu wa Usalama wa Milki za Ardhi kwa wananchi.

‘‘Ongezeko la idadi ya watu limeongeza kasi ya ukuaji wa vijiji vyetu na baadhi ya vitovu vya vijiji kubadilika kuwa vijiji miji hasa Chala, Kirando, Kabwe Asilia, Kipili na maeneo mengine hivyo uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi kwa kushirikiana na wananchi kutapunguza au kumaliza kabisa kwa migogoro ya ardhi, kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii na utunzaji wa mazingira’’ alisema Komba.

Aidha aliwataka Waheshimiwa Madiwani wote, Watendaji wa Kata na Vijiji kutoa ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha utekelezaji wa Uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji.

Nae Meneja Mradi Msaidizi Urasimishaji Vijiji Bw. Patrick Mwakilili amesema kuwa mradi umejikita katika kutoa elimu ya kwa wananchi kwa kuzingatia makundi mbalimbali yakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wanawake, vijana, wenye ulemavu sambamba na utoaji wa elimu ya usawa wa jinsia katika umiliki wa Ardhi ili kuhakikisha usalama kwa kila kipande cha ardhi kwa Mtanzania.

Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi umedhamiria kuendelea kutoa elimu kwa wadau katika ngazi ya Kitaifa, Wilaya, Mtaa/Kijiji mpaka Kitongoji ambapo kupitia Mkutano huo wa Wadau katika ngazi ya Wilaya ambapo wadau hupata fursa ya kutoa maoni yao ili kuboresha utekelezaji wa mradi katika maeneo yao.

About the author

mzalendo