Featured Kitaifa

MBUNGE KEYSHA AGAWA MITUNGI 200 YA GESI KWA WATU WENYE ULEMAVU MKOA WA DODOMA

Written by mzalendo

 

Mbunge wa Viti maalum Mhe Khadija Shabani Taya (Keysha) akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi wakikabidhi mitungi 200 kwa watu wenye ulemavu mkoa wa Dodoma .

Na Mathias Canal, Dodoma

Mbunge wa Viti maalum Mhe Khadija Shabani Taya amempa tano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhimiza Nishati safi ya kupikia ikiwa ni agenda ya kumtua Mama kuni kichwani.

Hiyo ni miongoni mwa mkakati jumuishi wa kuhakikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili mpaka kufikia 2033 wananchi zaidi ya 80% wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi na mkaa ulioboreshwa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi 200 kwa watu wenye ulemavu mkoa wa Dodoma iliyofanyika jana tarehe 7 Aprili 2024, Mbunge Keysha amesema kilichofanyika ni mwendelezo wa kile ambacho amekuwa akikifanya kwa watu wenye Ulemavu ikiwemo kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi Changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Mbunge Keysha amemshukuru Rais Samia kwa kuwajali watanzania hususani watu wenye ulemavu nchini.

“Na Mimi ninapoendelea kusema pale Bungeni haina maana kwamba sifurahishwi na mambo ambayo yamefanywa lakini jinsi ambavyo changamoto zinapozidi kutatuliwa ndivyo ambavyo changamoto zingine zinaendelea kuonekana, hatuna nia mbaya, nia yetu ni kujenga” amekaririwa Mhe Khadija

Katika hafla hiyo iliyoambatana na chakula cha jioni ikiwa ni sehemu ya iftar iliyofanyika katika viwanja vya CCM Mkoa wa Dodoma Mbunge Khadija ameiomba Serikali kurejesha asilimia mbili ambayo anaamini kuwa ni ukombozi kwa watu wenye ulemavu katika kujikwamua kimaisha na kiuchumi.

“Uzuri Naibu Waziri wa Tamisemi yupo hapa, naomba katika Halmashauri zetu Asilimia mbili peke yake zitawasaidia wajasiriamali, lakini kuna masuala ya mafuta ya watu wenye ualbino, kuna Vifaa kama (wheelchair), fimbo za watu wasioona n.k, tunaomba Ofisi yenu kupitia Halmashauri zenu ziendelee kutoa Vifaa ili maisha yetu yawe rahisi”

Mhegi rasmi katika hafla hiyo-Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira, Vijana na watu wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada mbalimbali katika kuwahudumia watu wenye ulemavu na wao kama Wizara wataendelea kufanya jitihada mbalimbali kuwazingatia watu wa Kundi hilo.

“tumefungua mfuko maalum kwaajili ya watu wenye ulemavu, Khadija Taya amefanya kazi hiyo na Fedha tayari tuna Shilingi Bilioni Moja kwa ajili ya watu wenye Ulemavu”

Mhe. Katambi amempongeza Mbunge Keisha kwa Jambo hilo la kufuturisha alilolifanya ambalo linatokana na upendo mkubwa alionao kwa wananchi.

“Alichokitoa hapa sio futari wala sio maji au soda, ametoa upendo wa dhati na moyo wa kujitoa tumekula upendo wake, tumekula matumaini yake, tumekula imani kubwa aliyonayo kwenu tumlipe hiyo kwa kuendelea kumfanya kuwa Kiongozi wetu, imani huzaa imani” Amesema Naibu Waziri Katambi

Kwa Upande wake mwakilishi wa Mufti Shekh Harith Nkussa amewasisitiza watanzania na hususani Waislamu kutoa mahitaji mbalimbali kwa watu wenye mahitaji maalumu kama alivyofanya Mbunge Keisha.

Mbali na Viongozi hao wa Serikali ibada hiyo imehudhuriwa pia na Wabunge mbalimbali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

About the author

mzalendo