Featured Kitaifa

ZAIDI YA MILIONI 60 ZAJENGA VIZIMBA VYA KUZUIA MAMBA BUCHOSA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Wizara ya Maliasili na Utalii  imetumia zaidi ya shilingi milioni 60 kujenga vizimba viwili kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya Mamba katika vijiji vya Kanyala na Izindabo kwenye tarafa ya Buchosa wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Hayo yamebainishwa leo Bungeni Jijini Dodoma na Mhe. Dunstan Kitandula wakati akijibu swali la Mhe. Eric Shigongo Mbunge wa Buchosa ambaye alitaka kujua kuhusu mpango wa Serikali wa kuendelea kujenga uzio katika sehemu za kuchota maji ili kuzuia vifo vinavyosababishwa na mamba Buchosa.

Mhe. Kitandula amesema kuwa Wizara ina mikakati ya ya aina mbili kwa ajili ya uvunaji wa mamba, mkakati wa kwanza ni kuvuna Mamba kwa njia ya uwindaji wa kitalii, lakini pia wizara inapopata taarifa ya Mamba wasumbufu kwenye maeneo ya wananchi wizara huwavuna mamba hao kwa ajili kuzuia maafa kwa wananchi. 

Aidha, ameongeza kuwa Wizara inatoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge kuzihimiza Halmashauri zao kutenga Fedha kwenye bajeti za Halmashauri zao zitakazowezesha ujenzi wa vizimba katika maeneo ya Halmashauri zao, na kwamba Wizara ipo tayari kutoa wataalam kwa ajili ya kutoa taaluma na kusimamia ujenzi wa vizimba hivyo.

About the author

mzalendo