Featured Kitaifa

TANZANIA NA DEMARK KUSHIRIKIANA KATIKA KUKUZA UCHUMI KUPITIA SEKTA BINAFSI

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof Kitila Mkumbo (Mb.), amefanya mazungumzo na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo na Sera za Mabadiliko ya Tabianchi wa Serikali ya Denmark, Mhe. Dan Jørgesen na kujadili masuala mbalimbali yaliyolenga kuimarisha ushirikiano katika maandalizi na utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo na uwekezaji.
Aidha, wawili hao wamejadili kuhusu mchakato wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambapo Mhe. Prof. Mkumbo amemueleza Mhe. Dan Jørgesen kwamba Serikali imekamilisha tathmini ya awali ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na sasa inashirikisha kikamilifu na wananchi katika maandalizi ya Dira mpya.
Vilevile, mazungumzo yao yaliangazia namna nchi hizi mbili zinavyoweza kushirikiana katika sekta mbalimbali za uwekezaji na biashara ikiwa ni pamoja na kuweka msisitizo kwenye kujengea uwezo kwa vijana katika masuala ya ujuzi ili waweze kujiajiri na kuzalisha ajira kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana.
Pamoja na mambo mengine, Waheshimiwa Mawaziri wamejadili juu ya ushirikiano utakaojikita katika kurasimisha sekta isiyo rasmi nchini ili kunyanyua uchumi wa Tanzania.
Tanzania na Denmark zimekuwa katika ushirikiano wa muda mrefu katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, miundombinu, uwekezaji na biashara.

About the author

mzalendoeditor