Ugonjwa wa wa macho mekundu au macho ya waridi (conjunctivitis) unaendelea kuongezeka nchini Malawi, na zaidi ya kesi 13,400 za ugonjwa huo zimeshathibitishwa tangu mwezi Februari mwaka huu wakati kesi za kwanza iliporipotiwa katika wilaya ya Karonga ya kaskazini mwa Malawi.
Ugonjwa wa Macho Mekundu ni hali ya inayosababishwa na kuvimba kiwambo cha sikio na tishu nyembamba na safi ambayo hufunika tabaka la juu la jicho.
Ugonjwa huo unasababishwa na vitu mbalimbali vikiwemo virusi ambavyo huenea kwa urahisi kutoka kwa mtu hadi mtu mwingine. Huwa vinaathiri jicho moja au yote mawili na ugonjwa huo unaweza kudumu hadi wiki mbili. Kujiikinga na ugonjwa huo kunafanyika kwa kunawa mikono mara kwa mara na kuepuka kugusa macho.
Ugonjwa huo hivi sasa umeenea kwenye wilaya 26 kati ya 28 za Malawi. Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wa afya wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika ambao wameongeza kuwa, hadi Jumamosi, jumla ya kesi 13,419 za ugonjwa huo zilikuwa zimeshasajiliwa.
Hakuna vifo vilivyoripotiwa hadi hivi sasa, ingawa kesi za matatizo ya kuona zimeripotiwa katika baadhi ya wilaya, hasa Karonga. Mapema mwezi Machi, Waziri wa Afya wa Malawi, Khumbize Kandodo Chiponda, aliwashauri wananchi kuepuka kupeana mikono na kuchunga usafi ili kuzuia kuenea zaidi ugonjwa huo.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kubadilika rangi ya macho na kuwa nyekundu au ya waridi katika sehemu nyeupe ya jicho, kuwashwa na macho, machozi ya mara kwa mara, uvimbe wa ukingo wa jicho, usumbufu wa kuona na matatizo mengineyo.