Featured Kitaifa

DKT.MFAUME AONYA UDANGANYIFU WA TAKWIMU KWA WATAALAMU WA AFYA

Written by mzalendo

OR-TAMISEMI

Mkurugenzi wa Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amewataka wataalamu wa Afya ya msingi kutoingia katika tamaa ya kudanganya takwimu za wagonjwa walio katika matibabu jambo ambalo ni kinyume na miiko ya kitaaluma.

Dkt. Mfaume ametoa maelekezo hayo baada ya kukagua shughuli za uendeshaji na usimamizi shughuli za Afya katika kituo cha Afya Mwandoya wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu akiwa ameambatana na timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI.

“Suala la takwimu ni muhimu sana tuzingatie kama wateja waliopima HIV ni wachache tuseme hivyo, tusijiingize katika vishawishi na matamanio ya kudanganya takwimu sasa wewe unadanganya ili umnufaishe nani na sio maadili kwenye kada ya Afya ni hatari sana na kinyume na miiko ya kitaaluma tukigundua hatutasita kuchukua hatua,” amesema Dkt.Mfaume

Aidha, ameielekeza timu ya uendeshaji wa shughuli za Afya ya wilaya (CHMT) ya Meatu kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ya kutembelea meneo ya kutolea huduma za Afya ikiwemo Vituo vya Afya na Zahanati mara kwa mara ili kushauri na kusimamia huduma za Afya.

About the author

mzalendo