Featured Kitaifa

RAIS SAMIA NI KINARA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO – MAJALIWA.

Written by mzalendo

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Wanananchi waliojitokeza kushiriki Kongamano la Miaka Mitatu ya Utendaji wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lililofanyika Katika Ukumbi wa Tunza Beach Jijini Mwanza.

……

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara na kielelezo cha utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoigusa jamii ya Watanzania.

Amesema kuwa maono na misingi  iliyojengwa na Rais, Dkt. Samia imewezesha Serikali ya awamu ya sita kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya kimkakati na kuimarisha utoaji wa huduma za jamii.

“Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji kwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kuimarisha usafiri wa anga, usafirishaji kwa njia ya reli, barabara na usafiri katika bahari na maziwa makuu”.

Amesema hayo leo (Jumamosi, Machi 30, 2024) wakati wa Kongamano wa Maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia lililofanyika Mkoani Mwanza.

Aidha,  amesema kuwa katika utekelezaji wa miradi ya usafiri katika maziwa makuu Serikalk imeendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa meli ya Mv. Mwanza Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1200, tani 400 za mizigo, magari madogo 20 na malori matatu na hadi sasa umefikia asilimia 94 ya ujenzi wake.

Amesema sambamba na ujenzi wa meli katika maeneo mbalimbali, Serikali pia imefanya maboresho katika bandari na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma katika bandari hizo ikiwemo bandari kwenye Ziwa Victoria. 

Ameongeza kuwa  katika kuimarisha Sekta ya kilimo, Serikali imeendelea kuboresha usimamizi na utoaji wa huduma  kwa kuongeza Bajeti katika Wizara ya Kilimo.

“Serikali imeweka msisitizo katika usimamizi wa zao la Pamba ikiwemo kuongeza thamani ya zao hili nitoe wito kwa wakulima wa zao hili kuongeza uzalishaji ili mahitaji tuliyonayo yaendane na uhitaji uliopo”.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa mradi wa Bandari ya Uvuvi pamoja na kutoa zana bora, pembejeo na vifaa muhimu vitakavyowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi lengo ni kuhakikisha sekta hiyo inachangia Pato la Taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja ikiwemo utekelezaji wa

“Katika kuimarisha Sekta ya uvuvi Rais amewezesha kununuliwa na kusambaza boti 160 za kisasa za uvuvi zenye thamani ya shilingi bilioni 11.5 kwa vyama vya ushirika wa wavuvi, watu binafsi na vikundi vya wavuvi katika Halmashauri 58.”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Wafanyabiashara wa Tanzania kutumia fursa za uwekezaji zilizowekwa na Serikali ya awamu ya sita ili kukuza uchumi wa Nchi na uchumi wao binafsi.

Naye,  Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa huo amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha Sekta ya elimu, afya na miundombinu.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jukwaa la Mafiga Matatu,  Aloyce Nyanda amesema kongamano hilo ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa wa miradi uliyotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania nzima kwa ujumla.

Kongamano hilo limehudhuriwa na watu wa kada mbalimbali ikiwemo wabunge, wahadhiri, watumishi wa Serikali, wafanyabiashara na wanafunzi wa vyuo mbalimbali jijini Mwanza ambao walipata nafasi ya kuchangia mada na kuuliza  maswali.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza Ndugu. Michael Lushinge Wakati alipowasili katika ukumbi wa Tunza Beach Jijini Mwanza kwa ajili ya kushiriki Kongamano la Miaka Mitatu ya Utendaji wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala. Leo 30 Machi 2024.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifuatilia wachangiaji mada wakati wa Kongamano la Miaka Mitatu ya Utendaji wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lililofanyika Katika Ukumbi wa Tunza Beach Jijini Mwanza Leo 30 Machi 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Wanananchi waliojitokeza kushiriki Kongamano la Miaka Mitatu ya Utendaji wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan lililofanyika Katika Ukumbi wa Tunza Beach Jijini Mwanza.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akichangia Fedha wakati wa harambee iliyofanywa  na Mlezi wa Wamachinga Stendi ya Nyegezi Bi. Beatrice Bahebe wakati wa Kongamano la Miaka Mitatu ya Utendaji wa Rais Samia Suluhu Hassan, lililofanyika Katika Ukumbi wa Tunza Beach Jijini Mwanza Leo 30 Machi 2023

About the author

mzalendo