Featured Kitaifa

TANZANIA YAKARIBISHA WAWEKEZAJI SEKTA YA NISHATI

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amesihi wawekezaji kutoka Mataifa mbalimbali (USA) kuwekeza katika sekta ya nishati nchini ikiwemo eneo la nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu pamoja na gesi ili kuendelea kuchochea maendeleo katika nyanja tofauti tofauti.

Kauli hiyo imetolewa Machi 27, 2024 katika Ofisi Ndogo ya Wizara iliyopo jijini Dar es Salaam alipofanya kikao na Naibu Waziri mdogo wa Nishati wa Marekani, Mhe. Joshua Volz kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko

Mhe. Kapinga amesema kuwa Tanzania ni sehemu salama ya kuwekeza hususan katika Sekta ya Nishati ambapo ameeleza kuwa Tanzania ipo tayari kupokea wawekezaji katika sekta ya nishati ili kuongeza tija kwenye maendeleo ya Nchi.

‘’Tanzania ina vyanzo vingi vya umeme ikiwemo nishati jadidifu kama vile Upepo, Jua na Jotoardhi, ndio maana nachukua nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchi ya Marekani wajitokeze kuwekeza katika sekta ya nishati hapa nchini,” amesema Mhe. Kapinga.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya umeme inayotokana na Nishati Jadidifu kama vile Mradi wa umeme Jua Shinyanga ambao unatarajia kuzalisha megawati 150 baada ya kukamilika, Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia Upepo uliopo Singida na Miradi ya Jotoardhi iliyopo katika Mikoa ya Songwe na Mbeya.

Mhe. Kapinga amesema Tanzania inaendelea na hatua za utekekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao unategemea kuzalisha jumla ya megawati 2,115 na utekelezaji wake umefikia asilimia 96.

Pia, Viongozi hao wamejadiliana kuhusu utekeleza miradi ya kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme inayotekelezwa nchini ili kuhakikisha umeme unafika maeneo mbalimbali nchini na kuvutia wawekezaji katika nyanja tofauti tofauti, pia wemezungumzia miradi kusafirisha umeme kati ya Tanzania na nchi nyingine.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani, Mhe. Joshua Volz ameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini ikiwemo miradi ya umeme na gesi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Mambo ya Nje,Viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati ya Marekani na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.    

About the author

mzalendo