Featured Kitaifa

WANANCHI SASA KUPATA BARUA YA UTAMBULISHO KIELETRONIKI BILA KWENDA KWA SHEHA

Written by mzalendo

Na. James K. Mwanamyoto – Unguja

Mhandisi wa Mifumo wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia Bw. Medson Naftali amesema Serikali imewawezesha wananchi kupata huduma ya barua ya utambulisho kieletroniki kupitia mfumo wa kidijitali wenye kanzidata ya anuani za makazi (NaPA) bila kwenda ofisini kwa sheha.

Bw. Naftali amesema hayo Unguja wakati akitoa mafunzo kwa wadau kuhusu namna barua ya utambulisho inavyopatikana kupitia mfumo wa NaPA, wadau ambao upokea barua za utambulisho katika shehia ya kizimkazi, dimbani na gulioni ambazo zimechaguliwa kufanya majaribio ya kutoa barua za utambulisho kieletroniki.

Bw. Naftali amewajengea uwezo wa namna ya utoaji na upokeaji wa barua ya utambulisho kidijitali, ambazo wananchi huziwasilisha katika taasisi zao ili kupata huduma walizokusudia.

“Hivi sasa serikali imechakata mfumo wa kidijitali unaomuwezesha mwananchi kuomba barua ya utambulisho sehemu yeyote alipo bila kulazimika kwenda ofisini kwa sheha,” Bw. Naftali amesisitiza.

Aidha, Bw. Naftali amewajengea uwezo wadau hao wa namna ya kupokea na kujiridhisha na barua hizo za kielektroniki kama ni halali au sio halali pindi zinapowasilishwa na wananchi katika taasisi zao ili kupata huduma stahiki.

Akitoa neno la shukrani baada ya kupokea mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mjini Magharibi Bw. Mbaraka Kasonfo amewasisitiza wadau hao, pindi wakirejea katika vituo vyao vya kazi kuwajengea uwezo wenzao ili utekelezaji wa zoezi la majaribio ya kutoa na kupokea barua za utambulisho kielektroniki lifanyike kikamilifu.

Kwa upande wake, mshiriki wa mafunzo hayo Bi. Amne Rashid ambaye ni Afisa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar amesema kuwa mafunzo ya utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi yatawasaidia kutambua maeneo yenye vyazo vya mapato ambavyo vitaongeza pato la nchi kupitia makusanyo ya kodi.

Naye, Mwinyi Ramadhan ambaye ni Afisa Takwimu wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mjini Magharibi amesema, kitendo cha mwananchi kuwezeshwa kuomba barua kielektroniki ni jambo zuri kwani Serikali imewarahisishia kupata huduma hiyo pasipokuwa na usumbufu wa kwenda kwenye ofisi za masheha, hivyo ameipongeza serikali kwa hatua hiyo muhimu.

Zoezi la kutoa barua za utambulisho kwa njia ya kielektroniki kupitia mfumo wa kidijitali wenye kanzidata ya anwani za makazi (NaPA) liko kwenye hatua ya majaribio katika kipindi cha miezi mitatu, ambapo kwa Unguja shehia ya Kizimkazi, Dimbani na Gulioni zimechaguliwa kwa majaribio.

About the author

mzalendo