Featured Kitaifa

DKT. BITEKO ASISITIZA KUIMARISHWA KWA MIFUMO YA UFUATILIAJI NA TATHMINI YA HUDUMA ZA AFYA YA MSINGI

Written by mzalendo


Na Gideon Gregory, Dodoma.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesisitiza suala la kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya huduma za afya ya msingi ili kuweza kufahamu maendeleo ya utekelezaji wa Afua mbalimbali za afya na kutambua maeneo ya kuboresha.

Dkt. Biteko amesisitiza hilo leo Machi 25,2024 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa Kimataifa wa Afya ya Msingi nchini Tanzania.

Aidha ufunguzi huo umeambatana na uzinduzi wa namba namba 115 ya kuwasiliana na watoa huduma kupitia mfumo wa M-mama unaoratibiwa katika hospitali za mikoa kupitia waratibu waliopewa mafunzo kwa ambapo kila mkoa wanaweza kutoa huduma hizo.

“Napenda kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo Vodacom Tanzania, Vodafone Foundation, USAID, Benki ya Dunia na wadau watekelezaji wa mfumo wa ‘Touch Health’ na ‘Pathfinder International’ kwa mchango wao katika kushirikiana na Serikali kuleta huduma hii inayohitajika kwa wote,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Sambamba na hilo ameagiza kuwekwa Mpango Mkakati wa kuhakikisha uwekezaji wa miundombinu uliofanywa na Serikali katika vituo ngazi ya Afya ya Msingi inatunzwa huku akiongeza kuwa miundombinu bora inawezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa urahisi zaidi.

Amesema, serikali imeweza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma ambapo kuanzia mwaka 2017 hadi Januari 2024, jumla ya vituo 2,799 vimejengwa na vingine kufanyiwa ukarabati, zikiwemo Zahanati 1,762, Vituo vya Afya 910, na Hospitali za Halmashauri 127.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Godwin Mollel amesema kuwa wataalam wa sekta hiyo wamejitoa kuhakikisha wanatoa huduma bora ya afya nchini hususan ya msingi na kuwataka washikamane kujenga sekta hiyo muhimu.

Naibu Waziri, Ofisini ya Rais, TAMISEMI, Dk.Festo Dugange, amesema hadi kufikia Februari mwaka 2024, Sekta ya afya ya msingi nchini Tanzania ina jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 6,933 zikiwemo Zahanati 5,887 Vituo vya afya 874 na Hospitali za Halmashauri 172.

“Takwimu hizi zinaonyesha kwamba kuna ongezeko kubwa la vituo katika Afya ya msingi ikilinganishwa na idadi ya vituo 5,270 katika mwaka 2015. Hii ni hatua kubwa katika kuelekea kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote nchini Tanzania,”amesema.

Amesema kwa mwaka, 2023, wateja milioni 26.9, walipata huduma katika vituo vya afya ya Msingi kama wagonjwa wa nje yaani (OPD), wateja 854,318 walipata huduma ya kulazwa (IPD). Katika eneo la mama na Mtoto wateja milioni 1.6 walijifungulia katika vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi na akinamama waliokuwa na uzazi pingamizi wakafanyiwa upasuaji walikuwa ni 125,318.

About the author

mzalendo