Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo amewahimiza wananchi kuhifadhi mazingira ili
kuwezesha upatikanaji wa maji hapa nchini.
Amesema kuwa uhai wa vyanzo mbalimbali vya maji vilivyopo nchini
unategemea uwepo wa mazingira yaliyohifadhiwa na kulindwa.
Mhe. Dkt. Jafo amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Kilele cha Wiki
ya Maji Tanzania na Siku ya Maji Duniani jijini Dodoma leo Machi 22,
2024 ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Waziri Dkt. Jafo amesema kuwa ajenda ya upandaji wa miti milioni 1.5
kwa kila halmashauri kwa kila mwaka ni ya muhimu kwani miti
ikipandwa kwa wingi ndipo vyanzo vya maji vinaongezeka.
Ameeleza kuwa kwa mwaka huu tayari miti zaidi ya milioni 260
imepandwa katika halmashauri hizo hivyo amewashukuru Wakuu wa
Mikoa na Wilaya kwa kuhamasisha upandaji wa miti katika halmashauri
zao.
Aidha, Waziri Dkt. Jafo ameipongeza Wizara ya Maji kwa kuwa mstari wa
mbele katika kufanya Tathmni ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya
kutekeleza miradi ya maji kwenye maeneo mbalimbali nchini.
“Nimshukuru sana Waziri wa Maji (Mhe. Jumaa Awesu) kwani wizara
yake na Ofisi yetu tunashirikiana kwa ukaribu sana katika utunzaji wa
mazingira ya mabonde na hata kule Mbeya tulipokutana tuliweka
mikakati kwa taasisi zilizo chini yetu namna gani zinaweza kushirikiana
katika ajenda ya kutunza mazingira,“ amesema.
Mhe. Dkt. Jafo amesema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea
kusimamia vyema mazingira kwani yakiwa salama ndio uhakika wa
upatikanaji wa maji kwa ajili ya uhai wa viumbe.
Amezungumzia kuhusu maadhimisho hayo ambapo amefafanua kuwa
Siku ya Maji imetokana na Mkutano wa Mazingira na Maendeleo kupitia
Azimio namba 47/193 lililootamka kuwa tarehe 22 ya mwezi Machi kila
mwaka Kuwa ni Siku ya Maji Duniani kupitia Mkutano wa Umoja wa
Mataifa (UNGA) mwaka 1993.