Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akihutubia wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na
Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro
tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akipanda mti aina ya Mdodoma katika Shule ya Sekondari Same
wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Upandaji Miti Kitaifa
iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango akikagua bidhaa mbalimbali zinazotokana na taka ngumu
zilizotengenezwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Manyinga ya mkoani
Morogoro kupitia mradi wa uhifadhi mazingira wa Eco School, wakati Makamu
wa Rais akikagua mabanda katika Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na
Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro
tarehe 21 Machi 2024.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amesema Serikali inazisisitiza Taasisi za utafiti wa misitu nchini
ziongeze kasi ya kufanya tafiti zinazolenga kutumia teknolojia kunusuru misitu
katika Taifa na kuongeza ustawi wake.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Misitu
Duniani na Upandaji Miti Kitaifa iliyofanyika katika Wilaya ya Same mkoani
Kilimanjaro tarehe 21 Machi 2024.
Amesema jitihada hizo zinapaswa kujumuisha tafiti kuhusu nishati safi ya kupikia ya gharama nafuu, nishati mbadala ya kukaushia tumbaku, kubuni bidhaa mbadala wa zile zinazotokana na miti au misitu na kuhuisha mbegu za miti ya asili.
Ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na
kituo cha Taifa cha kufuatilia hewa ya kaboni (National Carbon Monitoring
Centre) na OR-TAMISEMI kushirikiana na wadau ili kupata na kuasili teknolojia
za kisasa za kurahisisha ufuatiliaji na utoaji wa taarifa kwa wakati kuhusu
uharibifu wa misitu.
Makamu wa Rais ameagiza Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS)
kuhakikisha kila Halmashauri inaanzisha na kutunza vitalu vya miche ya miti
katika ngazi ya Halmashauri, kata na vijiji na kukamilisha kanuni za matumizi
ya misumeno ya minyororo (chain saw).
Aidha, amezitaka Halmashauri za Miji, Wilaya na Majiji kuanza kuchukua hatua za kuanzisha bustani za kijani (green parks) katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kupumzika, burudani na mazoezi ya viungo kwa wananchi.
Pia Makamu wa Rais amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kote
kuandaa na kusimamia utekelezaji wa mpango kazi wa kuhakikisha lengo
lililoelekezwa na Mhe. Rais la kuondoa matumizi ya nishati chafu ya kupikia
ifikapo mwaka 2030 linatimia. Amesema taarifa ya utekelezaji iwasilishwe
Ofisi ya Waziri Mkuu kila baada ya miezi sita.
Halikadhalika ameagiza Halmashauri zifanye jitihada za kujifunza kuhusu fursa
na changamoto zilizopo katika biashara ya kaboni pamoja na uendeshaji wa
biashara hiyo kutoka halmashauri zinazofanya vizuri kama vile Halmashauri za
Tanganyika, Karatu na Mbulu. Pia ameitaka Ofisi ya Makamu wa Rais –
Mazingira kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Wizara ya Maliasili
na Utalii na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia na kukamilisha
kanuni na taratibu zinazosimamia biashara ya kaboni hapa nchini haraka
iwezekanavyo.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Wilaya ya Same na maeneo jirani
kuzingatia maelekezo na ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kuhifadhi ardhi
na kunusuru Ziwa Jipe dhidi ya kujaa magugu ambalo ndiyo chanzo cha maji
cha Bwawa la Nyumba ya Mungu.
Vilevile Makamu wa Rais amesema Serikali itaongeza nguvu na uwezo wa
Taasisi za uhifadhi kuendesha doria za kudhibiti wanyama, kutoa mafunzo na
vifaa kwa wananchi kwa ajili ya kufukuza wanyama pori kwenye maeneo ya
wananchi katika vijiji vinavyokumbwa mara kwa mara na kadhia ya wanyama
kuharibu makazi na mashamba na hata kusababisha vifo.
Pia amesema Wizara ya Maliasili na Utalii ishirikiane na Wizara ya Fedha kuangalia upya kifuta machozi kwa wahanga wa uharibifu wa makazi, mashamba na vifo kutokana na wanyama hao.