Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa
Denmark nchini Tanzania Mhe. Mette Nørgaard Dissing-Spandet jijini
Dodoma leo Machi 18, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Denmark
nchini Tanzania Mhe. Mette Nørgaard Dissing-Spandet mara baada ya
kufanya mazungumzo jijini Dodoma leo Machi 18, 2024.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe.
Dkt. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Denmark
nchini Tanzania Mhe. Mette Nørgaard Dissing-Spandet (wa tatu kushoto)
mara baada ya kufanya mazungumzo jijini Dodoma leo Machi 18, 2024.
Na Mwandishi Wetu.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Dkt. Jafo amesema Tanzania inathamini
ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili na inatarajia kuendelea
kushirikiana zaidi katika hifadhi ya mazingira.
Amesema kuwa Tanzania inashirikiana na Denmark katika kusukuma
mbele ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo itasaidia
katika kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Kupitia ajenda hiyo amemtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ameonesha dhamira ya
dhati ya kuhakikisha asilimia kubwa ya wanawake wa Tanzania na Afrika
kwa ujumla wanatumia nishati safi ya kupikia.
Dkt. Jafo amesema kuwa katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa
Mabadiliko ya Tanianchi (COP28) uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu,
Rais Dkt. Samia alizindua Mradi wa Nishati Safi ya kupikia
itakayowasaidia wanawake barani Afrika.
Kutokana na umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, Waziri
Dkt. Jafo amesisitiza ni wakati sasa Tanzania inahitaji kuwabadilisha
wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuanza kutumia
nishati safi ya kupikia.
Ameongeza kwa kuwashukuru wawekezaji wa nishati safi ya kupikia
hususan gesi kwa kuunga mkono Serikali kwa kutoa mitungi ya gesi kwa
taasisi mbalimbali zinazolisha watu zaidi ya mia moja.
Halikadhalika, Dkt. Jafo amesema Tanzania inatekeleza mikakati
mbalimbali ya kukabiliana na athari za uharibifu wa mazingira ambapo
ilizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango Kabambe
wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032).
Kwa upande wake Mhe. Balozi Dissing-Spandet amemuhakikishia Waziri
Jafo kuwa nchi yake itaendeleza ushirikiano wake kwa Tanzania katika
sekta mbalimbali ikiwemo ya mazingira.