Featured Kitaifa

WAWILI WAHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Kagera.

Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba Mkoa wa Kagera imewahukumu washitakiwa Philbert Mukaru White (37), mkulima,mkazi wa mtaa wa Kagondo Kaifo Bukoba na Lameck Tuinomukama Martine (25), Fundi mkazi wa mtaa wa Kagondo Bukoba adhabu ya kunyongwa hadi kufa baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la mauaji ya Clavery Joseph Kamongo (25) dereva pikipiki (bodaboda) ambaye walimkodi kisha kumuua na kuiba pikipiki yake. 

Washitakiwa walitenda kosa hilo Julai 12,2020 majira ya saa nne kasoro robo usiku huko katika Kijiji cha Lwamulumba kata ya Karabagaine wilaya ya Bukoba vijijini Mkoani Kagera baada ya kumkodi awapeleke Bukoba mjini na walipofika maeneo ya vichaka ambako hakuna watu walimkamata kwa nguvu na kumnyonga shingo kwa kutumia waya waliokuwa nao wameuficha kwenye mavazi yao.

Akitoa hukumu hiyo March 13,2024 Jaji wa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba mheshimiwa Jaji Ngingwana amesema kuwa Mahakama Kuu kanda ya Bukoba imejiridhisha pasipo na shaka ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka na hatimaye kuwatia hatiani washitakiwa wote wawili kwa kosa la mauaji ya makusudi na wanastahili adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia hizo.

About the author

mzalendo