Featured Kitaifa

UCHUMI WA NCHI UNAENDELEA KUIMARIKA – DKT. MWIGULU

Written by mzalendo
Na. Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa Fadha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya kukumbwa na changamoto kadhaa ambazo baadhi zinatokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wa Serikali kama vile mabadiliko ya tabianchi, athari za vita na mabadiliko ya kisera za nchi zilizoendelea ikiwemo sera ya fedha ya kupunguza ukwasi katika uchumi.
Waziri Dkt. Mwigulu ameyasema hayo leo Machi 11,2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha katika kamati ya Bunge zima
mapendekezo ya mfumo na ukomo wa bajeti ya serikali
kwa mwaka 2024/25 ambapo emesema kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2023, ukuaji wa uchumi wa Taifa ulikuwa kwa 5.3%
ikilinganishwa na ukuaji wa 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.
“Katika mwaka mzima wa 2023 (Januari – Desemba), uchumi unatarajiwa kukua kwa wastani wa asilimia 5.2 ikilinganishwa na ukuaji halisi wa asilimia 4.9 mwaka 2022 mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi ni matokeo ya uongozi thabiti wa Serikali ya awamu ya Sita,”amesema.
Sambamba na hayo amesema mwenendo mzuri wa ukuaji wa uchumi ni matokeo ya uongozi thabiti wa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua jitihada mbalimbali za kukuza uchumi ikiwemo kuimarisha mazingira ya utawala bora na utawala wa sheria, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara, hususan utashi wa kisiasa wa kuruhusu mijadala na mashauriano ya masuala ya uwekezaji kwa wadau wa ndani na nje, kuongeza rasilimali fedha katika sekta za uzalishaji na huduma za jamii, na utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye matokeo ya haraka katika ukuaji wa uchumi, na kuendelea kutoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayoibuliwa na Serikali.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa lengo la Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25 ni kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi ambao ni jumuishi, unaopunguza umaskini na kuleta ustawi kwa wote, unaozalisha ajira kwa wingi, na unaochochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.
“Lengo la Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2024/25 ni kuendelea kuchochea kasi ya ukuaji uchumi ambao ni jumuishi, unaopunguza umaskini na kuleta ustawi kwa wote, unaozalisha ajira kwa wingi, na unaochochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi,”amesema.
Amesema kuwa katika kufikia shabaha hiyo msukumo utawekwa katika kuongeza tija ya uzalishaji na uongezaji wa thamani wa mazao katika sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, misitu na madini; kuchochea na kuboresha ubora wa elimu na mafunzo katika ngazi zote, kuongeza na kuimarisha matumizi zaidi ya teknolojia, hususani teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kuongeza uzalishaji viwandani; na kuimarisha huduma bora za jamii kwa wote, ikiwemo huduma za afya na upatikanaji wa maji safi na salama kwa wote.  
Sanjari na hayo Prof. Mkumbo amesema kuwa malengo na shabaha za uchumi kwa ujumla ni kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la Taifa kufikia 5.4% mwaka 2024 kutoka matarajio ya ukuaji wa 5.2% mwaka 2023.
“Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 7.0 katika muda wa kati, mapato ya ndani kufikia asilimia 15.7 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 15.3 mwaka 2023/24 mapato ya kodi kufikia asilimia 12.8 ya Pato la Taifa mwaka 2024/25 kutoka matarajio ya asilimia 12.5 mwaka 2023/24”,amesema.
Naye Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azan Zungu amesema jukumu la wabunge ni kupokea taarifa hiyo, hivyo hakutokuwa na mjadala wowote.

About the author

mzalendo