Kitaifa

PRST NA TAGCO YAKABIDHI MAPENDEKEZO YA SHERIA YA KUSIMAMIA TAALUMA YA UHUSIANO WA UMMA

Written by mzalendo

Dodoma

Chama cha Maofisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST) na Chama cha Maofisa Uhusiano na Mawasiliano Serikalini (TAGCO) wamekabidhi mapendekezo ya kuwa na Sheria itakayosimamia Taaluma ya Uhusiano na Umma (PR) na Mawasiliano kwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw.Mohammed Khamis Abdulla

Makabidhiano hayo yamefanyika leo tarehe 11 Machi, 2024 kwenye ofisi ndogo ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari jijini Dodoma.

Makamu wa Rais wa PRST Mary Kafyome na Makamu Mwenyekiti wa TAGCO Nteghenjwa Hosseah wamesema kwamba upo umuhimu mkubwa wa kuwa na sheria hiyo ambayo pamoja na mambo mengi itaanzisha bodi ya ithibati (Accreditation Board) ili kuwa na wanataaluma wenye weledi, uwajibikaji na sifa kwa maendeleo ya taifa.

Mbali na mapendekezo ya sheria, PRST pia, imemkabidhi Katibu Mkuu nakala ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Chama cha Maafisa Uhusiano na Mawasiliano Afrika Mashariki (EAPRA) ambayo Tanzania imechaguliwa kuwa Makao Makuu ya Chama hicho. 

Chama hicho chenye malengo makubwa ya kusaidia jumuiya katika Mawasiliano ya Kimkakati kimeundwa na vyama vya kitaaluma vya Uhusiano na Mawasiliano kutoka nchi wanachama Afrika Mashariki ambazo ni Public Relations Society of Tanzania (PRST, Public Relations Society of Kenya (PRSK), Public Relations Association of Uganda (PRAU) na South Sudan Public Relations Society (SSPRS).

About the author

mzalendo