Serikali ya Ethiopia imetoa takwimu zake rasmi na kusema kkuwa, takriban watu 1,358 wamefariki dunia katika ajali za barabarani nchini humo kwenye kipindi cha miezi sita iliyopita.
Waziri wa Mawasiliano wa Serikali ya Ethiopia, Selamawit Kassa, amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kuwa, ajali mbaya za barabarani zimezusha hofu na wasiwasi mkubwa katika nchi hiyo ya mashariki mwa bara la Afrika.
Amesema kuwa, hicho ni kiwango cha juu kabisa cha vifo vilivyosababishwa na ajali za barabarani katika kipindi cha miezi sita ya mwaka huu wa fedha wa 2023-2024 ulioanza Julai 8, 2023.
Ameongeza kuwa, mbali na kupoteza maisha idadi hiyo kubwa ya watu nchini Ethiopia, idadi ya majeruhi pia ni kubwa kiasi kwamba, watu wengine 2,672 wamepata majeraha mabaya kutokana na ajali hizo za barabarani katika muda huo.
Ameongeza kuwa, nchi kama nchi imepata hasara ya zaidi ya dola milioni 33 za Kimarekani kutokana na ajali hizo.
Kwa mujibu wa Waziri Kassa, uchunguzi unaonesha kuwa madereva ndio wa kulaumiwa kwa zaidi ya asilimia 60 ya ajali za barabarani nchini humo kutokana na uendeshaji mbaya, wa fujo, kutochunga sheria za barabarani na masuala mengine.
Ripoti zinaonesha kuwa, ustawi wa kiuchumi umeongezeka nchini Ethiopia na watu wa tabaka la kati na linalostawi nao wameongezeka hivyo wana uwezo wa kujikimu kimaisha na kuwa na vyombo binafsi vya kusafiria kama magari. Ongezeko hilo la magari limezusha mgogoro wa ajali nyingi na maafa yanayotokana na ajali hizo kwa upande wa mali na roho za watu.