Featured Kitaifa

WAZIRI MKUU AWEKA JIWE LA MSINGI SOKO LA KISASA TARIME MJINI

Written by mzalendo

 

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifungua kitambaa kuashiria ujenzi wa soko la kisasa katika halmashauri ya mji Tarime, wakati wa ziara yake Mkoani Mara, Februari 28, 2024. Soko hilo limegharimu shilingi bilioni 9.68. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Muonekano wa soko la kisasa katika halmashauri ya mji Tarime ambalo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko hilo, wakati wa ziara yake Mkoani Mara, Februari 28, 2024. Soko hilo limegharimu shilingi bilioni 9.68. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu akikagua maendeleo ya ujenzi wa soko la kisasa katika halmashauri ya mji Tarime baada kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko hilo, wakati wa ziara yake Mkoani Mara, Februari 28, 2024. Soko hilo limegharimu shilingi bilioni 9.68. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Tarime Mjini wakati wa ziara yake Mkoani Mara, kwenye viwanja vya shamba la bibi, Februari 28, 2024. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

…….

*Ujenzi wake kugharimu sh. bilioni 9.6, kukamilika Mei, 2024

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa soko la kimkakati la Tarime mjini unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 9.6 hadi kukamilika kwake.

Akipokea taarifa ya ujenzi wa soko hilo jana jioni (Jumatano, Februari 28, 2024) Waziri Mkuu alielezwa kwamba mradi huo kwa sasa upo katika hatua ya umaliziaji na umefikia asilimia 82 ya utekelezaji.

Akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tarime, Bi. Gimbana Ntavyo alisema shughuli zinazoendelea kwa sasa ni skimming, upakaji wa rangi, ufungaji wa milango kwenye maduka na vyoo na ufungaji wa mifumo ya umeme na maji kwenye jengo kuu la soko.

Alisema kazi nyingine ni uwekaji wa vigae na terazo kwenye vizimba, maduka ya nje na ndani na kwa upande wa kazi za nje, wanaendelea na uzalishaji wa paving na kuandaa maeneo ya kuzipanga.

“Hadi sasa malipo yaliyofanyika kwa mkandarasi ni sh. bilioni 5.77 na kwa mshauri ni sh. milioni 120.36 sawa na asilimia 60.86 ya gharama za mradi,” alisema na kuongeza: “Mradi huu utakuwa na maduka 325, vizimba 160, mabucha matatu, migahawa miwili, supermarket moja na Benki mbili.”

Akielezea manufaa ya mradi huo, Mkurugenzi huyo alisema mradi huo umetoa ajira za muda kwa watu 441 na utakapokamilika, Halmashauri inatarajia kuongeza mapato yake ya ndani kwa sh. milioni 588 kwa mwaka kutokana na mapato yatakayokusanywa.

About the author

mzalendo