Kitaifa

SERIKALI YASAINI MIKATABA UPEMBUZI YAKINIFU WA KUJENGA MELI ZA UVUVI NA BAHARI KUU NA UJENZI WA VIWANDA VYA KUCHAKATA SAMAKI

Written by mzalendo

Na. Mwandishi Wetu, Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi amewataka wataalamu waelekezi kutoka Kamapuni za DMG na TANSHEQ walioshinda zabuni ya Mkataba wa Upembuzi Yakinifu wa Ununuzi wa Meli za uvuvi wa Bahari Kuu na Ujenzi wa Viwanda vya Kuchakata Samaki,kukamilisha upembuzi kwa wakati ili Serikali ianze ujenzi wa meli katika Bahari Kuu na Viwanda vya kuchakata samaki.

Dkt . Yonazi ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma baada ya zoezi la utiaji saini wa Mikataba ya kufanya upembuzi yakinifu wa kijenga Meli za Uvuvi wa Bahari Kuu na viwanda vya kuchakata samaka vitakavyojengwa Kilwa na Fungurefu.
Amesema kuwa Mkataba huo utatekelezwa kwa muda wa siku zisizozidi 45 kwa gharama ya Shilingi milioni 348.

Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi ni ya kimkakati katika kuendeleza sekta ya kilimo na uvuvi, hivyo, katika zoezi hilo la upembuzi yakinifu ni vyema likasimamiwa kwa karibu ili kuhakikisha linafanyika kwa ufanisi unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zote zitakazojitokeza.

“Ni vyema mkafahamu kuwa, Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi ni moja ya Programu za kitaifa za kimkakati zilizo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020,” alisema.

Aliongezea kuwa programu hiyo inatija hasa kwa Viongozi Wakuu wa Nchi ambapo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania na Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wanaifuatilia kwa karibu. Lengo ni kuimarisha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa, pamoja na kuendeleza uchumi wa buluu.

“Kazi hii ifanyike kwa weledi na kukamilisha kwa wakati uliopangwa mtakuwa mmeshiriki katika kutafsiri maono ya Viongozi wetu hao wakuu.” Ameeleza Dkt. Yonazi
Amesema kukamilika kwa upembumbuzi yakinifu kwa wakati kutawezesha Serikali kuanza taratibu za ujenzi wa meli za uvuvi katika bahari kuu pamoja na viwanda vya kuchakata samaki vya Kilwa Na Fungurefu.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya AFDP Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Bw. Salimu Mwinjaka amesema kuwa matarajio ya Programu hiyo ni kuwanufaisha watu takribani 1,300,000 ikiwemo kaya za wakulima wadogo 200,000 amabao watakuwa wanapata mbegu bora za mahindi , alizeti na maharage.

Pia itawanufaisha wazalishaji wadogo na kati wa mbegu na wafanyabiashara za pembejeo za kilimo takribani 1,000 ambao watapata mbegu bora na mafunzo na wavuvi wadogo na wafanyabiashara wa samaki takribani 48,000 pamoja na wafugaji wa samaki na viumbe maji na mwani 21,000.

Amesema Serikali inakusudia kununua Meli 8 kwa ajili ya uvuvi wa Bahari Kuu ikijumuisha Meli 4 kwa ajili ya TAFICO na Meli 4 kwa ajili ya ZAFICO ambapo Zaidi ya Tsh Bilioni 30 kutumika kununua Meli hizo katika awamu mbili ambapo awamu ya kwanza kutakuwa na Meli 3 na Meli 5 zitanunuliwa katika awamu ya pili na meli hizo zinakusudiwa kuendeshwa kwa njia ya PPP.

About the author

mzalendo