Featured Kitaifa

DKT. BITEKO AAGIZA UBORESHAJI HUDUMA ZA AFYA KWA WAZEE

Written by mzalendo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa tatu kulia) akikabidhi kadi ya bima ya afya kwa mmoja wa wananchi kati ya 6000 waliofaidika na kadi za bima ya afya ambazo zimtolewa na Taasisi ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini tarehe 24 Februari 2024.

………………….. 

Azindua ugawaji Kadi za Bima ya Afya kwa wananchi 6000 jijini Mbeya

Mbeya kufaidika na mradi wa umeme wa TAZA

Vijiji 503 vyasambaziwa umeme

Mbeya

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa maelekezo kwa wasimamizi wa vituo vya Afya, Zahanati na Hospitali zote nchini kuhakikisha wanayasimamia madirisha ya Wazee kwa weledi ili yaweze kutoa huduma bora kama ilivyo kwa makundi mengine ya wananchi.

Ametoa maelekezo hayo tarehe 24 Februari 2024 jijini Mbeya katika hafla ya kukabidhi kadi za bima ya afya kwa wananchi takriban 6000 ambazo zimetolewa na Taasisi ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini.

“Wazee hawa walilinda amani ndio maana tukakuta Taifa lenye amani, waliunda mshikamano tukakuta Taifa lenye mshikamano, tusiwavunje moyo watakapokuja kwetu kupata huduma, watendeeni wema wazee hawa, wapeni huduma bora na muone fahari ya kuwa na wazee wenye afya njema nchini.” Amesema Dkt. Biteko

Kuhusu utoaji wa Kadi za Bima ya Afya kwa wananchi jimboni Mbeya Mjini, Dkt. Biteko amempongeza Mhe.Dk.Tulia Ackson kwa moyo wake wa upendo na dhamira njema aliyonayo katika kuwasaidia watu wa Mbeya na kwamba nia hiyo njema ni somo kwa walio wengi hasa Wabunge.

Akizungumzia  Sekta ya Nishati, Dkt. Biteko ameendelea kusisitiza kuwa, changamoto za umeme zinakera viongozi wote wakuu wa nchi pamoja na wananchi ambapo ameahidi kuwa sasa zimefika ukingoni na hali  inaendelea kutengemaa kupitia uendelezaji wa vyanzo vipya vitakavyoingiza umeme kwenye Gridi ikiwemo mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao muda wowote kuanzia sasa utaingiza megawati 235 katika Gridi ya Taifa.

Kuhusu hali ya umeme mkoani Mbeya, Dkt. Biteko amesema kuwa changamoto ya umeme mkoani humo inasababishwa na upungufu wa umeme katika gridi na gridi yenyewe kwani miundombinu ya umeme wa gridi inaishia mkoani Mbeya ambayo ina umbali mrefu kutoka kwenye vyanzo vya umeme hivyo athari yoyote ikitokea kwenye njia ya umeme inaathiri watu waliopo mwishoni.

 Amesema Serikali iliamua kujenga mradi wa usafirishaji umeme wa kV 400 wa Tanzania -Zambia ( TAZA) wenye thamani ya shilingi Trilioni 1.4 ambapo mradi huo utahusisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme jijini Mbeya.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa vituo vya kupoza umeme utafanyika pia katika maeneo mengine mkoani Mbeya ikiwemo Makongorosi na Uyole kwani lengo ni Mkoa wa Mbeya kupata umeme wa uhakika ambao hausafiri kwa umbali mrefu.

Amesema kuwa, mahitaji ya umeme mkoani Mbeya ni megawati 70 ambapo kwa wiki iliyopita upungufu wa umeme mkoani humo ulikuwa ni megawati 37 hadi 40 na hivyo kupelekea  kupata umeme kidogo. Hata hivyo ameeleza kuwa hali inaendelea kutengemaa kwani kwa takwimu za leo asubuhi upungufu wa umeme mkoani humo ni megawati 20.

Kuhusu usambazaji wa umeme vijijini amesema kuwa, Mkoa huo una Vijiji 533 ambapo Vijiji vilivyosambaziwa umeme ni 503  huku Vijiji 30 vilivyosalia, wakandarasi wakiendelea kusambaza umeme.

Aidha, amesema kuna vitongoji 2,951 ambapo vitongoji ambavyo vimeshasambaziwa umeme ni 1,953 na kazi ya kusambaza umeme kwenye vitongoji vilivyosalia inaendelea.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametaka watendaji katika Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) kusimamia ipasavyo vyanzo vya umeme nchini  ikiwemo Maji, Jotoardhi, Upepo na Jua ili kuwa na umeme wa kutosha.

Vilevile,  Dkt. Biteko amewaasa wananchi wa Mbeya kupendana na kushirikiana ili  Mkoa wa Mbeya uwe bora na wenye maendeleo na hivyo wasiruhusu tofauti za makabila, madhehebu au itikadi za vyama kuwatenganisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema kuwa, huduma zimeendelea kuboreshwa mkoani humo ikiwemo za Afya ambapo Halmshauri zote  zina Vyumba maalum kwa ajili ya matibabu ya wazee wote.

Ameongeza kuwa, Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitendea haki Mbeya kwa kuimarisha miundombinu mbalimbali kama vile ujenzi wa uwanja wa kimataifa wa ndege wa kilometa 3.3 ambao sasa unarahisisha usafiri kwa wananchi ndani na nje ya Mkoa.

Pia amemshukuru Dkt. Samia kwa mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka eneo la Igawa wilayani Mbeya hadi  Tunduma na barabara ya mchepuko kwenda mkoani Songwe ambayo itarahisisha huduma za usafiri ndani ya nchi na kwa magari yanayoenda nje ya nchi.

Awali, Mkurugenzi wa Taasisi yaTulia Trust, Mhe. Dkt.Tulia Ackson alisema kuwa, huduma za afya katika Jimbo hilo zinaendelea kuimarishwa na sasa kuna zahanati, vituo vya afya, Hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Hospitali ya Kanda ambazo zinatoa huduma kwa wananchi wa ndani na nje.

Amemshukuru  Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma hizo za afya na Sekta nyingine.

Dkt. Tulia amesema kuwa, bima hizo zinazotolewa na Taasisi ya Tulia zitawawezesha wananchi kupata matibabu hadi ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa.

Taasisi ya Tulia imekuwa na utaratibu wa kutoa bima hizo za afya kwa Wazee, Watu wenye ulemavu na kaya zenye uhitaji ambapo kutoka mwaka 2019 hadi sasa jumla ya kaya 2670 zimefaidika  huku idadi ya wananchi wakiwa ni 16,020 na zoezi hilo linaendelea. 

About the author

mzalendo