Featured Kitaifa

UTEKELEZAJI MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI WAFIKIA 70%-KATIBU MKUU MOHAMMED KHAMIS ABDULLA

Written by mzalendoeditor

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohammed Khamis Abdulla amesema utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya Kidijitali umefikia asilimia 70 na utekelezaji wake ni wa miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.

Amesema mradi huo una malengo ya kuchochea mabadiliko ya kidijitali nchini, uundwaji wa mfumo wa namba moja ya utambulisho (jamii namba) mbayo itatumika kufanya utambuzi kuanzia mtu anapozaliwa ili kumwezesha mwananchi kupata huduma mbalimbali zikiwepo za afya, elimu, usafiri na nyinginezo pamoja na kuunganishwa katika mifumo ya vitambulisho vya Taifa, vyeti vya kuzaliwa na vinginevyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mjini Zanzibar kuhusu mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Abdulla amesema pamoja na mambo mengine, mradi huo pia utawezesha uundwaji wa mfumo wa kitaifa na uunganishwaji wa mifumo (National Enterprises Service Bus) utakaounganisha mifumo ya serikali na binafsi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Tunalenga kuendelea kuboresha mfuko wa anwani za makazi na postikodi ili kuwezesha watoa huduma mbalimbali nchini, kuweza kutambua wateja wao kielektroniki na kuondoa adha ya mwananchi ya kwenda kila mara kuomba utambulisho kwenye serikali za mitaa, pia mradi huu utawezesha kupeleka mawasiliano ya mtandao wa simu kwenye maeneo ambayo hayakuwa na mawasiliano ambapo kwa sasa, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea na ujenzi wa minara mipya ya simu 438 na upandishaji wa hadhi minara 304” amesema Bw. Abdulla.

Aidha amebainisha kuwa mradi huo utawezesha kuunganisha taasisi za Serikali 891 na mtandao wa mawasiliano ya Serikali (GovNet), ili kufikisha mawasiliano ya kimtandao kwenye ofisi hizo, zinazojumuisha hospitali, vituo vya afya, shule, mahakama, vituo vya polisi, vituo vya halmashauri, na taasisi za serikali.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bi Khadija Khamis Rajab amesema Zanzaibar itanufaika na mradi huo kupitia marekebisho ya kanuni, sheria na sera ya TEHAMA ili kuendana na mabadiliko yake ambapo kwa sasa kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) tayari wamepata minara 42 ya mawasiliano.

“Kupitia mradi huu tutaweza kupata minara mingine ya nyongeza katika maeneo ambayo bado hayajaweza kufikiwa vizuri kwa upande wa mawasiliano, na hii tutafanya kutokana na ripoti ambazo tutazipata kupitia kwa wenzetu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wao watatuambia ni minara mingapi na ni kwenye maeneo gani inahitajika, pia tutaweza kuimarisha minara ya mawasiliano ili iweze kuwa bora zaidi, na maeneo yote yaweze kufikiwa na huduma za mawasiliano mijini na vijijini” amesema Bi. Rajab.

Amesema pia kutakuwa na mifumo 17 ambayo wataweza kunufaika nayo kupitia mradi huo kupitia vituo 159 ambavyo vitajumuisha shule, vituo vya afya, halmashauri na maeneo mengine ikiwemo taasisi za serikali.

Nae Afisa Mwandamizi wa Maendeleo ya kidijitali kutoka Benki ya Dunia Bw. Paul Seaden amesema lengo la Benki hiyo la kutoa Dola za Kimarekani milioni 150 ni kusaidia kuwezesha mradi huo ambao utaiwezesha Tanzania kuendelea katika mifumo ya mawasiliano ya kidijitali.

About the author

mzalendoeditor