Featured Kitaifa

DKT. BITEKO ATAKA MIUNDOMBINU YA UMEME KUBORESHWA KWA WAKATI

Written by mzalendo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
akizungumza mara baada ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Ikwavila
wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa nne
kushoto)  akikata utepe kuashiria uwashaji umeme katika Kijiji cha
Ikwavila wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka na wa tatu kutoka kulia Mbunge wa Wanging’ombe Dkt.Festo Dugange.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
(kushoto),  Mbunge wa Wanging’ombe Dkt.Festo Dugange (kulia) na Mkuu
wa Mkoa wa Njombe, Antony Mtaka  (wa kwanza kutoka kushoto) wakipiga
makofi mara baada ya kuwasha umeme katika Kijiji cha Ikwavila wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe.

……………………

Aagiza kituo cha kupoza umeme kujengwa Wanging’ombe

 Asema JNHPP imefikia asilimia 97

Ataka kigezo cha mavazi kisikwamishe watoto kwenda shule

Vijiji vyote 108 Wanging’ombe vyapata umeme

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amewaagiza wataalam kufanya ukarabati wa miundombinu ya umeme kwa
wakati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya umeme ya uhakika.

Dkt. Biteko amesema tabia ya  kutobadilisha au kukarabati miundombinu
kwa wakati pale inapoharibika inawakosesha wananchi  huduma ya umeme
kwa kipindi kirefu.

Amesema hayo tarehe 21 Februari, 2024  wakati wa ziara yake mkoani
Njombe ambapo amewasha umeme katika Kijiji cha Ikwavila na Shule ya
Sekondari ya Wasichana Njombe iliyoko wilayani Wanging’ombe pamoja na
kukagua mindombinu ya uzalishaji umeme na nguzo za umeme katika
kiwanda cha TANWAT.

Dkt. Biteko ametoa maagizo hayo baada ya Mbunge wa Wanging’ombe, Mhe.
Dkt. Festo Dugange kueleza kuwa, Wilaya hiyo ina changamoto ya radi
nyingi zinazosabababisha transfoma kuungua kwa takriban 50 hadi 60 kwa
mwaka lakini ubadilishaji wake umekuwa ukichukua muda mrefu na hivyo
kuathiri shughuli za kijamii na kiuchumi.

“Hili suala la transfoma inaungua halafu inachukua hadi mwezi mmoja
kubadiliswa, uzembe huu haukubaliki,  Idara ya Manunuzi TANESCO
tumeibadilisha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kama hii ya
uzembe wakati  vifaa hivi vinazalishwa kwenye viwanda vya ndani,
tunataka watendaji hawa waone shida wanazopata wananchi na kuzitatua,
kweli kuna changamoto ya umeme lakini kuna baadhi ya matatizo TANESCO
wanaweza kuyamaliza.”  Amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan hataki kero ya umeme
iendelee ndio mana utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere
(JHNPP) unaenda kwa kasi na sasa umefikia asilimia 97 na mtambo mmoja
umekamilika utakaoingiza megawati 235 kwenye gridi mwezi huu huku
mtambo mwingine ukitarajiwa kuingiza megawati nyingine 235 mwezi Machi
mwaka huu.

Kuhusu ombi la Mbunge wa Wanging’ombe kupata  laini ya umeme
inayojitegemea kwani laini ya sasa inatumiwa pia na eneo Lupembe na
TANWAT mkoani Njombe na hivyo kufanya umeme wilayani humo kuwa hafifu,
ameagiza TANESCO kujenga kituo cha kupoza umeme wilayani humo ili
kutengemaza hali ya upatikanaji umeme..

Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali imeamua kwa nia moja kuwaletea
maendeleo wananchi kwa kutekeleza miradi katika Sekta zote ikiwemo
Miundombinu, Nishati, Afya, Maji na ndio maana wilaya hiyo ya
Wanging’ombe imesambaziwa umeme kwenye vijiji vyote 108 na zaidi ya
asilimia 56 ya vitongoji wilayani humo vimesambaziwa umeme huku kazi
ikiendelea na kwamba shilingi Bilioni 9 zimetengwa kwa ajili ya
kusambaza umeme wilayani humo.

Katika hatua nyingine. Dkt.Biteko amewataka wananchi kutoruhusu
itikadi za vyama kuwagawanya hasa katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utakaofanyika mwaka huu na kusisitiza kuwa watumie uchaguzi huo
kuchagua viongozi wanaowaunganisha na kuwaletea maendeleo.

Aidha ameagiza viongozi mbalimbali wa Serikali kujikita kwenye kutatua
changamoto.za wananchi na kuwapelekea maendeleo na si kushughulikiana.

Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza kuwa, watoto wote wanaopaswa kuripoti
mashuleni wafanye hivyo na kuelekeza wasimamizi wa Elimu kuhakikisha
kuwa hakuna mtoto anayekwamishwa kuripoti shule kwa sababu ya kigezo
cha mavazi kama vile viatu kwani suala la msingi kwa watoto hao ni
elimu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Wanging’ombe, Mhe. Dkt. Festo Dugange
amempongeza Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya Afya, Elimu, Nishati na Maji katika
wilaya ya Wanging’ombe.

Kuhusu miradi ya umeme vijijini, ameishukuru Serikali kupitia Wizara
ya Nishati kwani vijiji vyote108 katika Wilaya ya Wanging’ombe vina
umeme na katika vitongoji 523 wilayani humo tayari vijiji 295 vina
umeme na kazi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vingine ikiendelea.

Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (
REA), Mhandisi Godfrey Chibulunje alisema kuwa, Mkoa wa Njombe
umetengewa shilingi biioni 70.44 kusambaza umeme vijijini huku
Wangingombe ikipata shilingi bilioni 9.35.
Kuhusu usambazaji umeme vijijini mkoani humo amesema.kuwa katika
vijiji 381 tayari vijiji 361 vina umeme sawa na aslimia 94.75

Katika vitongoji amesema kuwa Mkoa una vitongoji 1836 ambapo vitongoji
1148 vina umeme sawa na asilimia 62.5 huku kazi ya kusambaza umeme
kwenye vitongoji vilivyosalia ikiendelea.

Kwa nyakati tofauti viongozi mbalimbali wa Wilaya hiyo wamemshukuru
Dkt. Biteko kwa kuwa kiongozi wa kwanza kufika katika kijiji cha
Ikwavila na hii ikionesha jinsi anavyofuatilia utekelezaji wa miradi
kwa umakini.

About the author

mzalendo